………
Na Mwandishi Wetu-JKCI
22/8/2025 Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imetia saini ya makubaliano ya ushirikiano na Chama Cha Madaktari wa Moyo cha nchini Misri kuanzisha huduma za upimaji na matibabu ya magonjwa ya shambulio la moyo kwa wanamichezo ili kuzuia vifo vya ghafla michezoni.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge amebainisha hayo leo Agosti 22, 2025 wakati wa hafla ya utiaji saini ya ushirikiano huo mpya na kuongeza kuwa huduma hizo zitakuwa za kwanza kutolewa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na hivyo kusaidia kudhibiti vifo vya ghafla kwa wanamichezo.
“Tayari tumetia saini na Timu za Simba na Yanga, sasa tunaelekea timu ya Azam na baadae timu zote zinazoshiriki ligi kuu hapa Tanzania, pia tutaenda mbali kwa vyama vya riadha, gym na umma kwa ujumla ili kuwaellimisha kuwa wanapaswa kufanya vipimo vya moyo kabla ya kuanza mazoezi”, alisema Dkt. Kisenge na kufafanua kuwa
“Ukivunjika mguu utaugua miezi mitatu na baade kurudi uwanjani, lakini ukipata shindikizo la moyo unapoteza maisha, kusainiwa kwa makubaliano haya yamewezekana kutokana na uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba vya kisasa uliofanywa na Serikali ya awamu ya Sita katika taasisi yetu”.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Magonjwa ya Moyo cha nchini Misri, Prof. Ahmed Eissa alisema chama chake kitashiriki katika kuijengea uwezo JKCI kwa kuwafundisha wataalamu namna bora ya kutoa huduma hizo muhimu kwa wanamichezo.
“Misri tunauzoefu wa kutosha wa kutoa huduma hizi za matibabu ya moyo kwa wanamichezo hivyo tutawajengea uwezo madaktari wa hapa JKCI ili huduma hizi ziweze kuwafikia wanamichezo wengi na kupunguza vifo vya wanamichezo” alisema Prof. Eissa.
Naye Mratibu wa mpango huo wa JKCI Dkt. Eva Wakuganda alisema jumla ya watu milioni 300 wanatarajia kunufaika na huduma hiyo mpya katika nchi za Ukanda wa Kati na Mashariki ya Afrika.
“Wanamichezo wapo katika hatari kubwa ya kupata vifo vya ghafla vinavyotokana na magonjwa ya moyo, kupitia huduma hii tutashuka hadi ngazi ya shule kutoa elimu ya namna ya kuwasaidia wanamichezo wanaopata matatizo ya moyo wawapo michezoni”, alisema Dkt. Wakuganda.
Hafla hiyo ya utiaji saini iliambatana na maadhimisho ya miaka 10 ya utoaji huduma ya JKCI ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Mkuu wa Ubalozi wa Misri nchini Mhe. Amr Selim ambaye aliipongeza JKCI kwa mafanikio makubwa ya kutoa huduma bora za matibabu ya Moyo kwa Watanzania na kwamba nchi yake itaendelea kuunga mkono jitihada hizo.