Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH) Dkt. Luzila John akiwaangalia wataalamu wa afya jinsi wanavyowahudumia wananchi katika kambi maalumu ya ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa hospitali hiyo.
Dakatari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mlagwa Yango na wenzake wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH) wakiingiza taarifa za mkazi wa Shinyanga aliyefika katika hospitali hiyo kwaajili ya kupata huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa kwenye kambi maalumu ya matibabu inayofanyika SRRH.
Fundi sanifu wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Pascal Kondi akiwaelekeza madaktari namna ya kufanya kipimo cha kuagalia jinsi moyo unavyofanya wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH)
………….
Na Jeremiah Ombelo – JKCI, Shinyanga
22/08/2025 Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamewajengea uwezo wa jinsi ya kuwatambua na kuwatibu wagonjwa wa moyo wataalamu wa afya kutoka Hospitali mbalimbali zilizopo mkoani Shinyanga.
Mafunzo hayo kwa njia ya vitendo yanafanyika kwenye kambi maalumu ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga (SRRH).
Akizungumza na waandishi wa habari jana Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Luzira John alisema kambi hiyo imewajengea uwezo madaktari na wauguzi wa hospitali hizo wa kupima vipimo vya moyo na kutoa matibabu ya magonjwa ya moyo.
“Madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga pamoja na halmashauri zote za mkoa huu wamepata mafunzo kuhusiana na huduma za upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo, hii itawawezesha kutatua changamoto za wagonjwa mapema kabla hazijawa kubwa”, alisema Dkt. John.
Aidha Dkt. John alimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge kwa kujitoa kushiriki moja kwa moja kwenye kambi hiyo na kuwafundisha madaktari hao kwa siku tatu mfululizo.
“Kwa kipekee tunamshukuru sana Dkt.Kisenge kwa kuungana nasi ameonyesha mshikamano na kujitolea muda wake kuhudumia wananchi na pia kuwaimarisha wataalamu wetu”, alishukuru Dkt. John.
Kwa upande wake Daktari wa magonjwa ya ndani wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH) Neema Mmassy alisema wamepata mafunzo ya kiutendaji kutoka kwa madaktari bingwa wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jambo litakalowawezesha kutoa huduma bora hata baada ya kambi hiyo kumalizika.
“Tunashukuru uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutuletea madaktari bingwa wa moyo, hii imetujengea uwezo mkubwa kwa sababu magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo ni changamoto kubwa nchini”, alisema Dkt. Mmassy.
Naye Daktari wa watoto wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH) David Mwamfula alisema wamejengewa uwezo wa kutumia vifaa vya kisasa vya moyo vilivyoletwa na madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kufundishwa namna ya kutoa tiba bora kwa watoto wenye matatizo ya moyo.
“Ujio wao umetufundisha mambo mapya tumepata ujuzi wa kitaalamu na tumekutana na vipimo vipya vya moyo ambavyo hatukuwa navyo awali kama kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi”, alisema Dkt. Mwamfula.
“Kwa sasa idara yetu ya watoto imepata ujuzi mkubwa. Tumeelezwa namna ya kuwatibu watoto wenye changamoto za moyo za kuzaliwa nazo pamoja na wale waliopata matatizo ukubwani,” aliongeza Dkt. Mwamfula.
“Ujio wao umekuwa wa faida kubwa kwetu tumeongeza ujuzi na sasa tunaweza kuwahudumia wagonjwa wetu vizuri zaidi kwa sababu tumepata mbinu nyingi mpya kutoka kwao,” alisema Dkt. Happiness Malosha.