Na Issa Mwadangala.
Wananchi wa kata ya Itale Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe wamejengewa uelewa kuhusu faida za maendeleo ya kibiashara na fursa mbalimbali zinazotokana na mazingira mazuri katika miundombinu ya biashara wakati wa shughuli ya ufyatuaji wa matofali ukiendelea katika eneo ambalo wanajenga majengo ya biashara katika kata ya Itale kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa mahitaji na bidhaa katika kata hiyo.
Akizungumza Agosti 21, 2025 na wakazi wa eneo hilo, Polisi kata ya Itale Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Geofrey Suchile amewaasa wananchi kuwa kipaumbele katika shughuli za maendeleo, aliyasema hayo wakati aliposhiriki katika shughuli za ufyatuaji wa tofali kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya bisashara katika kata ya Itale tarafa ya Bulambya wilaya ya Ileje mkoa wa Songwe.
“Polisi Jamii inalenga kuimarisha mahusiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi, kwa kutatua changamoto mbalimbali za kijamii kwa njia ya ushirikiano. Wananchi ni walinzi wa kwanza wa amani na usalama katika maeneo yao.” alisema Mkaguzi Sichule.
Pia, Mkaguzi Sichule, alisema Jeshi la Polisi linahakikisha jamii inapata uelewa sahihi kuhusu nafasi yao katika kuleta maendeleo katika jamii zao kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu, na Jeshi la polisi litahakikisha usalama wa mali zao katika eneo hilo ambapo ujenzi wa majengo ya biashara unaendelea.
Mkaguzi Sichule, alihitimisha, kwa kuwaeleza wananchi hao kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuwahamasisha na kushiriki shughuli za maendeleo katika jamii zetu kama ujenzi wa masoko ili watu wajipatie fursa mbalimbali za kujipatia kipato kwa njia halali ili kupunguza matendo ya uhalifu miongoni mwa jamii zetu.