Na Sophia Kingimali.
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Albert chalamila ametoa rai kwa wananchi kutunza afya zao kwa kutumia nishati safi ya kupikia huku wakichukua dhana hiyo ya matumizi ya nishati safi kama agenda ya Taifa.
Wito huo ameutoa leo Agosti 22,2025 katika kongamano la Pika kijanja msimu wa nne lililoandaliwa na Shirika la utangazaji TBC kupitia redio yake ya Bongo Fm lengo likiwa kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya nishati safi lakini pia kuibua fursa zitokanazo na matumizi ya nishati hiyo.
Amesema afya ni mtaji sahihi kwa maisha ya kila binadamu hivyo kila mmoja anapaswa kuwa barozi wa nishati safi kwa kuhakikisha anatumia na kahamasisha wengine kutumia ili kulinda Afya lakini pia kutunza mazingira.
“Ishikeni dhana ya nishati safi kama agenda ya Taifa yenye manufaa kwako wew mwenyewe lakini kwa Taifa na uharibifu wa mazingira unaoufanya sasa madhara yake yataathiri mpaka vizazi vijavyo”,Amesema Chalamila.
Akizungumzia kuhusu Uchaguzi Mkuu Chalamila amewasihi wananchi kuhakikisha wanalinda amani ya Taifa pia kujitokeza kupiga kura na kuchagua viongozi kutokana na sera zao.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Daphrosa Kimbory, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Ayub Rioba Chacha, amewapongeza vijana wa Bongo FM waliobuni kampeni ya Pika Kijanja, akisema imekuwa na matokeo chanya katika kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya nishati safi.
Pia ameahidi kuhakikisha agenda ya nishati safi inafika kila sehemu nchini ili kufikia adhama ya Rais mpaka kufikia 2034 asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati hiyo kwa kuendelea kuandaa makongamano ya kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Nae,Mkuu wa Bongo Fm Annastazia Willherick amesema kupitia redio yake ya Bongo FM itaendelea kuibeba ajenda ya kitaifa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambayo mwasisi wake ni Rais Samia Suluhu Hassan, hadi mwaka 2034 ambapo inatarajiwa Watanzania asilimia 80 watakuwa wanatumia nishati hiyo.