Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Magingo Halmashauri ya Madaba Wilayani Songea wakifuatilia warsha iliyoandaliwa na Taasisi ya Alpha Tanzania iliyolenga kuhamasisha wanafunzi kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao(Picha na Muhidin Amri)
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Madaba Wilayani Songea Mkoa wa Ruvuma,wakifuatilia mada mbalimbali kwenye warsha ya kuwajengea uwezo wanafunzi wa shule za Sekondari zilizopo katika Halmashauri ya Madaba iliyoandaliwa na Taasisi ya Alpha Tanzania yenye Makao Makuu Nchini Taiwani(Picha na Muhidin Amri)
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba Mkoani Ruvuma Joseph Mrimi,akimsikiliza mkulima wa Parachichi wa Kijiji cha Magingo Evaristo Nyoni kushoto, namna miche ya zao hilo inavyooteshwa kwenye maonyesho ya bidhaa za kilimo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Alpha Tanzania yenye makao makuu Nchini Taiwani,kulia ni Mkurugenzi wa Taaisi hiyo Grace Mayemba(Picha na Muhidin Amri)
Mkurugenzi wa Taasisi ya Alpha Tanzania yenye makao makuu nchini Taiwan Grace Mayembaa,akizungumza kwenye warsha ya kuwajengea uwezo wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari katika Halmashauri ya Madaba Mkoani Ruvuma iliyofanyika katika kijiji cha Magingo(Picha na Muhidin Amri)
…………..
NA MWANDISHI MAALUM, MADABA
Shirika lisilo la Kiserikali la Alpha Tanzania lenye makao makuu nchini Taiwan limetenga zaidi ya Shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi wa kujenga Shule ya Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza katika Kijiji cha Magingo, Kata ya Mkongetema, Halmashauri ya Madaba, Wilaya ya Songea.
Ujenzi wa shule hiyo ni sehemu ya dhamira ya shirika hilo kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha sekta ya elimu nchini, hususan kusaidia watoto wanaotoka katika mazingira magumu na familia zenye kipato cha chini ili wapate elimu bora itakayowawezesha kutimiza ndoto zao.
Akizungumza na wanafunzi, walimu na wazazi katika warsha ya kuwajengea uwezo wanafunzi wa shule za sekondari za Lipupuma, Magingo na Madaba, Mkurugenzi wa Shirika hilo Grace Mayemba alisema yeye na marafiki zake walioko Taiwan wamejipanga kuhakikisha ujenzi wa shule hiyo unaanza haraka ili watoto wa familia maskini wapate fursa ya elimu na ujuzi wa kuwasaidia katika maisha.
“Mpaka sasa tumefanikiwa kukusanya zaidi ya Shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi, pia tumekuja na viti 100 na meza 100. Hata hivyo hatujaanza ujenzi kama tulivyokusudia kwa sababu taasisi yetu bado haijakamilisha usajili. Mara tu baada ya usajili kukamilika, ujenzi utaanza mara moja,” alisema Mayemba.
Aidha, alibainisha kuwa tayari wamepata ekari 10 kutoka Serikali ya Kijiji cha Magingo, lakini mahitaji halisi ni kati ya ekari 50 hadi 100 ili kuwezesha mipango ya kujenga shule, hoteli, viwanja vya michezo, chuo cha ufundi na hospitali kwa ajili ya jamii ya Madaba na Mkoa mzima wa Ruvuma.
“Lengo kubwa ni kusaidiana na Serikali kuboresha elimu na huduma za kijamii ili vijana wapate elimu bora, afya na ujuzi utakaowawezesha kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Mayemba, mradi huo unakuja kujibu changamoto ya kata ya Mkongetema kutokuwa na shule ya mchepuo wa Kiingereza kwa watoto wanaotoka katika familia duni. Pia alisema mpango wa kujenga chuo cha ufundi utasaidia vijana ambao hawajapata nafasi ya kuendelea na elimu ya juu kupata ujuzi wa kitaaluma.
“Nimepata nafasi ya kusoma nchini Taiwan na nilipoishi huko nilikuwa na ndoto ya kutoa mchango katika jamii niliyotoka. Nimewashirikisha marafiki zangu tisa na wote wamekubali kuunga mkono ndoto hizi, tukianzia hapa kijiji cha Magingo,” alisema Mayemba.
Amewaomba viongozi wa Serikali kuharakisha mchakato wa usajili wa taasisi hiyo kwani marafiki wake tayari wameanza kuchangia fedha lakini changamoto ni kukosa akaunti rasmi ya kuhifadhi michango hiyo.
Mwakilishi wa marafiki hao kutoka Taiwan, Angle Kwok, alisema wanatambua changamoto zinazowakabili vijana wa Madaba na Tanzania kwa ujumla, na hivyo wako tayari kushirikiana na Mayemba kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Joseph Mrimi, aliipongeza Alpha Tanzania kwa kuonyesha moyo wa kujali wananchi, hasa vijana wanaokwamishwa na changamoto za kifamilia na kiuchumi.
“Serikali inatambua na kuthamini mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika kuharakisha maendeleo ya nchi yetu. Ni faraja kubwa kuona wazawa wetu wa Madaba wanakumbuka nyumbani na tuko tayari kushirikiana nanyi ili malengo yenu yatimie,” alisema Mrimi.
Aliongeza kuwa Halmashauri ya Madaba bado inakabiliwa na mahitaji makubwa ya miundombinu bora ya elimu na afya, huku Serikali ikiendelea kutenga fedha kila mwaka ili kuboresha huduma hizo kwa wananchi.
Wakazi wa Kijiji cha Magingo pia wameeleza kufurahishwa na mradi huo, wakisema utakuwa na manufaa makubwa kwa jamii. Lucy Chondota, mkazi wa kijiji hicho, alisema shule na chuo kitakapokamilika, wazazi wengi wataweza kuwapeleka watoto wao kupata elimu bora bila gharama kubwa.
Naye Evaristo Nyoni, mkulima wa eneo hilo, alisema mradi huo utasaidia kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa kuongeza soko la mazao yanayozalishwa kijijini hapo.