Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
SERIKALI imeziagiza halmashauri za majiji, miji na wilaya zipatazo 34, kuwapeleka watumishi wanamichezo kushiriki Mashindano ya Shirikisho Michezo ya Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA) yanayofanyika mkoani Tanga.
Agizo hilo limetolewa leo Agosti 23, 2025 na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe Zainab Katimba, alipokuwa akifungua mashindano ya 40 ya SHMISEMITA yanayohudhuriwa na halmashauri 150 kati ya 184 zilizopo nchini.
Kabla ya ufunguzi huo, taarifa ya SHIMISEMITA iliyosomwa na Katibu wake wa Taifa, Henry Kapella, ilitoa rai kwa mamlaka husika, kuzichukulia hatua halmashauri zilizoshindwa kuwagharamia watumishi wao kushiriki mashindano hayo, kwamba ni sawa na kuwanyima haki ya kujihusisha na kupata burudani kupitia michezo.
Pia, Kapella amesema jitihada za kukuza na kuendeleza michezo nchini, zinapaswa kuakisiwa na utengaji wa bajeti ya kutosha ili halmashauri zimudu kugharamia mipango ya tasnia hiyo kwenye maeneo yao.
Akitoa agizo hilo, Mhe Katimba amesema michezo ni sehemu muhimu kwa uimarishaji wa afya ya akili na mwili, iliyotolewa maelekezo na viongozi wa ngazi na nyakati tofauti kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha watumishi wao wanashiriki SHIMISEMITA.
Kwa hali hiyo, Mhe Katimba amesema kwa kipindi cha wiki ijayo, halmashauri zote 34 ambazo haziwagharamia watumishi wake, zihakikishe watumishi wanamichezo wao wanafika mkoani Tanga kushiriki SHIMISEMITA ifikapo wiki ijayo.
Amesema ushiriki wa watumishi kwenye michezo kunachangia ukuzaji wa afya njema, ukakamavu, weledi, kujenga umoja, ushirikiano, uaminifu na mahusiano mazuri kazini na kwa wananchi wengine.
Mhe Katimba amesema, ndio maana Serikali imeendelea kutilia mkazo watumishi wake kuendeleza vipaji kwa kushiriki mashindano, ziara na mafunzo ya kimichezo katika ngazi za kitaifa na kimataifa.
Kwa upande mwingine, Mhe Katimba amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Majiji, Miji na Wilaya kurejea maagizo ya Serikali kwa nyakati tofauti, kufanikisha juhudi za kuimarisha utamaduni wa Mtanzania na michezo mahali pa kazi.
Amesema utekelezaji utafanikiwa kwa ikiwa Wakurugenzi hao watatenga fedha za kutosha kwenye bajeti kwa kitengo cha michezo, sanaa na utamaduni, kupitia mgawo wa kila mwezi.