
Jina la Damon Dash, maarufu kama 77 Dash, si geni katika tasnia ya muziki wa Tanzania, alianza kujizolea umaarufu kuanzia mwaka 2014 alipoanzisha na kusimamia kundi la Hip Hop lililojulikana kama BOB na Micharazo.
Kundi hili liliwakutanisha wasanii wanane wenye vipaji tofauti ambao ni Mr. Blue, Nyandu Tozzy, Becka Tittle, Blood Gaza, Baby MC, Uswege Master, Cotton, na Ivason.
Kupitia uongozi madhubuti na usimamizi wa 77 Dash, BOB na Micharazo waliweza kurekodi na kuachia nyimbo tatu zenye ushawishi mkubwa, Shut Up Kimya, Wamekaa, na Kazi Kwanza.
Ngoma hizi zilitikisa sana kwenye anga ya Hip Hop na kufanikiwa kuwagusa mashabiki wengi sana na chakuvutia zaidi, nyimbo hizi bado zinapata usikilizwaji mkubwa mpaka leo na zinapatikana kwenye majukwaa mbalimbali ya kidijitali, jambo linalozipa uhai hata katika enzi ya kisasa ya usambazaji wa muziki.
Ni muhimu pia kuelewa kuwa mchango wa 77 Dash haukuishia tu kwenye kuwaunganisha wasanii tu bali aliweza kutoa muongozo, dira na msaada wa kweli uliowezesha kundi hilo kustawi wakati ambao miradi ya pamoja ya Hip Hop haikuwa ya kawaida.
Ushawishi wake uliweka msingi ambao umeendelea kuwapa motisha watu wengi ndani ya tasnia ya muziki ndani na nje ya Bongo.
Hata nje ya kazi ya BOB na Micharazo, jina la Damon Dash limeendelea kutajwa sana katika medani pana ya muziki.
Msanii kama Young Lunya, ambaye ni mmoja wa vinara wa kizazi kipya cha Hip Hop Tanzania humtaja mara kwa mara kwenye sehemu za mwisho za nyimbo zao, wakimpongeza kwa mchango wake.
Wasanii kama Meja Kunta na wengine wamekuwa wakimtaja hadharani kama mtu aliyewasaidia kwa ushauri, msaada na motisha katika safari zao za muziki.
Kutajwa huku mara kwa mara na wasanii wa kizazi tofauti ni ishara ya wazi ya nafasi ya kudumu ya 77 Dash kama mlezi na mtetezi wa vipaji. Jina lake limekuwa kielelezo cha uvumilivu, uthabiti, na uwezo wa kuinua wengine.
Katika miaka ya hivi karibuni, pamoja na kudumu kwa jina lake katika muziki, 77 Dash amepanua malengo yake na kuingia kwenye biashara, hasa kwenye sekta ya madini.
Hatua hii inaonesha wazi roho yake ya uanzishaji biashara na uwezo wake wa kuwekeza katika maeneo tofauti nje ya burudani ni uthibitisho wa maono yake ya kutaka kuleta mabadiliko ya kweli na ya kudumu katika sekta mbalimbali.
Kwa kumalizia, Damon Dash, yaani 77 Dash ni mtu wa kipekee katika tasnia ya ubunifu Tanzania, mpambanaji aliyewajengea majukwaa wasanii, akaunda mwelekeo wa Hip Hop, na anaendelea kuhamasisha kwa kujitolea kwake na uongozi thabiti.
Leo hii anapogeukia biashara kubwa kama ya madini, bado anabeba azma na ujasiri ule ule uliomjenga katika muziki, jambo linaloihakikishia nafasi ya jina lake katika maeneo mengi ya jamii ya Tanzania.