▪️Wapongeza ugawaji wa Leseni kwa wachimbaji wadogo Singida
▪️Singida wavuka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli
▪️Waziri Mavunde aeleza mkakati wa kuongeza eneo la utafiti wa kina madini nchini
▪️Kampuni za madini zajipanga kuanzisha Mgodi Mkubwa wa Dhahabu kanda ya Kati (Dodoma & Singida)
📍 Iramba – Singida.
Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoa wa Singida wamepongeza jitihada kubwa za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya madini, ikiwemo kugawiwa leseni na kuwekewa mazingira bora ya kufanya kazi zao kwa amani.
Pongezi hizo zimetolewa leo Agosti 23, 2025 wakati wa Kongamano la Wachimbaji Wadogo wa Madini wa Mkoa wa Singida na Kanda ya Kati, lililofanyika katika eneo la Sekenke One, Shelui – Wilaya ya Iramba, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde.
Wachimbaji hao wameleza kuwa, hatua ya Serikali kufuta na kurudisha Serikalini leseni na maombi 2,648 ambayo hayakuwa yakifanyiwa kazi, kisha kugawiwa upya kwa wachimbaji wadogo, imekuwa suluhisho la muda mrefu kwa changamoto ya kuvamia maeneo na kuchimba bila leseni.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema mpango wa Serikali ni kuongeza kiwango cha utafiti wa kina wa madini kutoka asilimia 16 kilichopo sasa hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030, kupitia maono ya Vision 2030; Madini ni Maisha na Utajiri.
Amesema kuwa, Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 115 kwa ajili ya utafiti wa madini nchini, ikiwa ni pamoja na kununua helikopta maalum yenye vifaa vya kisasa kwa ajili ya upigaji picha na utafiti wa anga, sambamba na ujenzi wa maabara za kisasa za uchambuzi wa madini zitakazotumika na wachimbaji wadogo.
Wakati huohuo, Waziri Mavunde amebainisha kuwa Kampuni kubwa za madini zimeanza kujipanga kuwekeza katika Mgodi mkubwa wa dhahabu katika Kanda ya Kati (katika mikoa ya Dodoma na Singida), hatua inayotarajiwa kuongeza zaidi fursa za ajira, mapato ya Serikali na mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), Bw. John Bina, alisema zaidi ya wachimbaji wadogo milioni 6 wanashiriki kikamilifu katika shughuli za madini na wamefanikisha sekta hiyo kuchangia hadi asilimia 40 ya mapato yote ya madini nchini.
“Tunampongeza Rais Samia kwa maono yake ya kuendelea kuithamini sekta ya wachimbaji wadogo. Hii ni heshima kubwa kwetu na ndiyo maana leo tunasherehekea mafanikio haya,” alisema Bina.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, alisema sekta ya madini ndiyo inayoongoza kwa kasi ya ukuaji kiuchumi ndani ya mkoa huo na imewezesha Singida kuvuka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.
“Madini ndiyo injini ya uchumi wa Singida, na kwa sasa mchango mkubwa unatoka kwa wachimbaji wadogo waliowekewa mazingira bora ya kufanikisha kazi zao,” amesema.
Awali, akizungumza katika kongamano hilo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Mhandisi Sabai Nyansiri, amesema mkoa huo umefanikiwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali yatokanayo na sekta ya madini katika mwaka wa fedha 2024/25, baada ya kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 26 dhidi ya lengo la shilingi bilioni 24.