Na Mwandishi wetu, Sanya Juu Kilimanjaro.
Jamii ya wamasai waliohamia katika kijiji cha Msomera kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wameshiriki tamasha la Kitamaduni na Kimila la Wamasai (Orkwaak le Maasae 2025), linalofanyika Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
Wananchi hao kutoka Msomera walihamia eneo hilo wakitokea hifadhi ya Ngorongoro wameungana na wananchi wengine wa kabila la kimasai kutoka maeneo mbalimbali nchini na kushiriki tamasha la Orkwaak le Maasae lenye lengo la kudumisha na kuenzi mila, desturi na urithi wa kitamaduni wa jamii ya Kimasai, kujifunza, kubadilishana maarifa na kuonesha utambulisho wao wa kitamaduni.
Akizungumza baada ya uzinduzi wa tamasha hilo lililokutanisha wananchi zaidi ya 30,000 , Bi. Juliana Thadei Saidimu, mkazi wa Msomera, amesema wanafurahi kuona kwamba wanakutana na wenzao kutoka mataifa mbalimbali kusherekea siku hiyo .
Kwa upande wake kiongozi wa kimila kutoka Msomera, Bw. Komba Riko Lodoo, alisema hatua ya serikali kuendelea na kushirikisha wananchi katika matukio ya kijamii na kitamaduni ni ushahidi kuwa, hata baada ya kuhamia Msomera, jamii hiyo bado imebaki thabiti katika kuenzi mila zao.
“Wananchi tuliotoka Ngorongoro kwenda Msomera sio kuwa tumekuwa huru katika uzalishaji wa Uchumi, kujitegemea, kupata huduma bora za kijamii lakini pia tunapata uhuru wa kufanya shughuli zetu za kimila kwa kuwa maeneo tunayo lakini pia tunapata fursa adhimu kama hii kushiriki na wenzetu kudumisha mila na tamaduni za kimasai kwa pamoja” alisema Laigwanan Lodoo.
Kupitia tamasha hili la siku tatu, jamii hiyo ya wamasai inaendeleza dhamira yake ya kulinda, kuhifadhi na kukuza urithi wa kitamaduni wa makabila ya Tanzania, ili kuhakikisha thamani ya mila na desturi inabaki kuwa urithi hai kwa Taifa.