Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na Wasimamizi wa maeneo mbalimbali ya kazi wa Taasisi hiyo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili yanayofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Abdulrahman Muya akizungumza na wasimamizi wa maeneo mbalimbali ya kazi wa taasisi hiyo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uongozi yaliyofanyika jana katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Baadhi ya wasimamizi wa maeneo mbalimbali ya kazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakisikiliza mada zilizokuwa zikiendelea wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uongozi uliofanyika jana katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha mkoani Pwani. Picha na JKCI.
………
Na Mwandishi Maalumu – Kibaha, Pwani
23 Agosti 2025 – Wasimamizi wa maeneo mbalimbali ya kazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kuwa walezi bora kwa watumishi wanaowaongoza ili kuongeza mshikamano wa kikazi, kuimarisha utendaji na kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wagonjwa.
Rai hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wasimamizi wa wa maeneo mbalimbali wa taasisi hiyo. Mafunzo hayo yanafanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Dkt. Kisenge alisema wasimamizi wa vitengo hukutana na changamoto mbalimbali za kikazi kutoka kwa watumishi wanaowasimamia, hivyo ni muhimu wawe walezi na viongozi bora ili kuwasaidia watumishi kutatua changamoto hizo na kufanikisha malengo ya taasisi.
“Mafunzo haya ya uongozi niliona myapate kwani nyie ni sehemu ya viongozi wa taasisi yetu. Mkitoka hapa mkayafanyie kazi mtakayoelekezwa na kuyatengenezea mikakati mizuri ili kuboresha huduma zetu”, alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Mkuu wa Utawala wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Priscilla Mkini alisema mafunzo hayo yataleta mabadiliko chanya katika utendaji kazi na kuimarisha mshirikiano kati ya wasimamizi na watumishi wanaowaongoza.
“Siku hizi mbili mkizitumia ipasavyo mtaweza kutimiza lengo lililowaleta hapa na kuwa viongozi bora kwa wengine”, alisema Mkini.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa JKCI, Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Watu Abdulrahman Muya alisema mafunzo hayo yamelenga kuwaunganisha wasimamizi wa vitengo ili kubadilishana uzoefu, kuimarisha mshirikiano na kupata ujuzi wa namna bora ya kuongoza watumishi.
Muya aliongeza kuwa washiriki wa mafunzo hayo watajifunza wajibu wao katika kusimamia rasilimali za umma, namna ya kutambua hisia za watu wanaowaongoza, uadilifu na kujenga ushirikiano kazini.
“Idara ya Utawala na Rasilimali Watu itaendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wafanyakazi ili kuimarisha utendaji. Ninaamini kwa pamoja tutaweza kufikia malengo tuliyojiwekea”, alisema Muya.