Fundi Mchundo wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke, Bw. Stephano Raymond, akikagua mita ya LUKU ya mteja katika eneo la Mbagala Zakhem, wakati wa utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya ukaguzi wa miundombinu ya umeme, iliyofanyika 22 Agosti 2025, Mbagala, Dar es Salaam.
……..
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke limewakamata baadhi ya wateja wake katika eneo la Mbagala Zakhiem kwa tuhuma za wizi wa nishati ya umeme pamoja na uharibifu wa miundombinu, ikiwemo kuharibu mifumo ya LUKU jambo ambalo ni kinyume cha sheria na taratibu za matumizi ya umeme.
Akizungumza leo, Agosti 21, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa Operesheni Maalum ya ukaguzi wa miundombinu, Fundi Mchundo wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Bw. Stephano Raymond, amesema kuwa ukaguzi huo umebaini kuwepo kwa vitendo vya uharibifu wa miundombinu na wizi wa umeme vinavyofanywa na baadhi ya wateja wasio waaminifu.
Bw. Raymond ameongeza kuwa watuhumiwa wote waliokamatwa wamefikishwa kwenye vyombo vya dola kwa hatua zaidi za kisheria, huku akisisitizwa umuhimu wa wananchi kufuata taratibu sahihi katika matumizi ya umeme ili kuepuka matatizo yasiyo ya lazima.
TANESCO Mkoa wa Temeke imeendelea na na operesheni hiyo katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo hadi pale vitendo vya hujuma na wizi wa umeme vitakapokoma.