
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limethibitisha tukio la mauaji ya raia wawili wanaosemekana kuwa ni kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), waliouawa kwa kupigwa na kuchomwa moto na wananchi katika Kijiji cha Chafuma, Kata ya Kapele, Tarafa ya Ndalambo, Wilaya ya Momba. Tukio hilo lilitokea Agosti 22, 2025, saa 8:00 mchana.
Marehemu hao wamefahamika kwa majina ya Babuloha, kijana mwenye umri wa kati ya miaka 26 hadi 28, na mke wake Jenifa Babuloha, mwenye umri wa kati ya miaka 23 hadi 25. Wanandoa hao walidaiwa kuhusika na mauaji ya mwenye nyumba wao, marehemu Imbanji Simwaka, mwanamke kikongwe mwenye umri wa miaka 80.
Kwa mujibu wa Polisi, Imbanji Simwaka aliuawa usiku wa Agosti 19, 2025 baada ya kukatwa kichwani kwa kitu chenye ncha kali, kisha mwili wake kufukiwa bafuni nyumbani kwake. Tangu Agosti 20, 2025 marehemu hakuwahi kuonekana, jambo lililozua hofu miongoni mwa ndugu na wanakijiji.
Mnamo Agosti 22, 2025 wananchi walipoanza kumtafuta marehemu, waligundua kaburi la siri bafuni kwake. Wakati huohuo taarifa zilienea kwamba wanandoa waliokuwa wapangaji wa marehemu walionekana wakiuza baadhi ya mazao yake, jambo lililoibua hasira kali kwa wananchi. Wanandoa hao walikamatwa na kukabidhiwa kwa uongozi wa kijiji ili taratibu za kisheria zichukuliwe.
Hata hivyo, kabla ya hatua hizo kufanyika, kundi la wananchi wenye hasira kali walivamia ofisi ya kijiji, kuwapora washukiwa na kuwaua kwa kutumia silaha za jadi kisha kuchoma miili yao moto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe amelaani vikali matukio yote mawili ya mauaji na kusisitiza kuwa kujichukulia sheria mkononi ni kosa kubwa kisheria na ni kitendo kinachohatarisha amani na usalama wa jamii.
Aidha, Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea ili kuwatambua na kuwakamata wote waliopanga, kushiriki au kuchochea tukio hilo la kikatili, na kuwasilisha majina yao mbele ya vyombo vya sheria.
Polisi wametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe kuepuka tabia ya kujichukulia sheria mkononi, na badala yake kutoa taarifa kwa vyombo husika wanaposhuhudia au kuwa na mashaka kuhusu vitendo vya uhalifu. Pia wamehimizwa kutokuwa tayari kuwapokea wageni wasiofahamika bila taarifa kwa viongozi wa kijiji ili taratibu stahiki zichukuliwe