Rombo. Mgombea ubunge Jimbo la Rombo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Profesa Adolf Mkenda, amechukua fomu ya kuwania tena nafasi ya ubunge katika jimbo hilo, akiahidi kufanya kampeni kwa kutembea kila kijiji ili kuomba kura ndani ya chama chake.
Agosti 23,2025 Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM Taifa (INEC), ilitangaza majina ya wagombea ubunge na uwakilishi kupitia chama hicho, kwa majimbo ya Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na viti maalum kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo leo, Agosti 24 2025, Profesa Mkenda ameishukuru Halmashauri Kuu kwa kumteua kuwa mgombea rasmi wa chama hicho.
Amesema atafanya kampeni kwa kushirikiana na wagombea wa nafasi nyingine ndani ya chama hicho ili kuhakikisha ushindi kwa CCM katika ngazi zote.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, Cornelia Bitegeko, amewakumbusha wagombea wote kujaza kwa usahihi na umakini fomu zinazotolewa na tume ya uchaguzi kutokana na maelekezo yaliyomo kwenye fomu hizo.