

Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) katika kuelekea Mkutano wao Mkuu wa Mwaka wanaenda sambamba na kufanya matendo ya huruma kwa kutoa misaada kwa jamii.
Leo wanachama wa taasisi hiyo wamepeleka misaada ya vitu mbalimbali kwa wafungwa na mahabusu wa Gereza Kuu la Ukonga Jijini Dar.

Akizungumza na wanahabari wakati za kukabidhi msaada huo mapema leo, Agosti, 24,2025 Mwenyekiti wa chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) Devotha George Mrope amesema katika kuelekea mkutano wao mkuu unaotarajia kuanza Agosti 25 mpaka 28 mwaka huu wameonelea kuanza na kufanya matendo ya huruma.
Katika kufanya hivyo juzi walienda kutoa msaada kwa wagonjwa wa moyo wa Taasisi ya Jakaya Kikwete JKCI iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jana walipeleka msaada Taasisi ya Kansa ya Ocean Road na leo wamefika Gereza Kuu la Ukonga kwa ajili ya kuwapelekea wafungwa msaada huo.
Devota amesema wafungwa ni sehemu ya wanajamii wetu hivyo nao wanahitaji faraja na upendo kwani si kila aliyeko gerezani ametenda kosa.
Wapo waliojikuta wakiingia gerezani kwa bahati mbaya na hata waliotenda makosa bado wanaweza kubadilika kitabia na kuwa raia wema na kuwa msaada kwa jamii yetu hivyo ni muhimu kuwajali kwani kutenda kosa si kosa bali kosa kurudia kosa. Amesema Devota.
Akielezea lengo la Mkutano Mkuu wa TRAMPA amesema la kwanza ni kusherehekea miaka 13 ya mafanikio ya taaluma ya chama hicho kilichopo chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwanachama wa chama hicho.
Devota amesema lengo lingine ni kufanya harambee ya kujenga ofisi ya TRAMPA ambayo itakuwa ni Kituo cha Maarifa na Ukumbi mkubwa wa mikutano na ofisi ya Masijala ya mfano.
Devota amesema lengo lingine kubwa na la mwisho ni kuwamashisha wananchi kwenda kushiriki uchaguzi mkuu wa ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Kwa upande wa Gereza Kuu la Ukonga, Mrakibu Mwandamizi Jeshi la Magereza Juma Kapilima aliwashukuru wanachama wa TRAMPA kwa msaada waliowapelekea na kusema japo serikali inafanya jitihada kubwa za kuyahudumia vizuri magereza yake kote nchini lakini hatuwezi kuzuia msaada.
Hivyo basi tunawakaribisha na wadau wengine kuja kutoa msaada kwani mahitaji siku zote huwaga hayana ukomo yataendelea kuhitajika tu.