Na Issa Mwadangala.
Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe wapongezwa kwa utendaji mzuri wa utoaji huduma bora kwa mteja.
Kamishna wa Polisi Jamii CP Faustine Shilogile amehimiza utendaji wenye weledi na Uadilifu wakati akizungumza na Watendaji wa Dawati hilo akiwa ziarani Mkoani Songwe Agosti 25, 2025.
CP Shilogile pamoja na ujumbe wake kwa watendaji hao, alipokelewa na tafrija maalum iliyopambwa na shampeni, kukata keki, pamoja na kupatiwa zawadi mbalimbali kama ishara ya shukrani na kuthamini mchango wao katika kulinda haki na ustawi wa watoto na wanawake.
Kamishna Shilogile, amepongeza juhudi za watendaji hao na kusisitiza kuwa mafanikio ya Dawati la Jinsia na watoto yanatokana na moyo wa kujitolea, uadilifu na uwajibikaji wa watumishi hao katika kutatua changamoto mbalimbali za kijinsia zinazowakabili wananchi.
Aidha, alisisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuwa bega kwa bega na dawati hilo katika kuhakikisha kuwa huduma bora na zenye haki zinafika kwa wahitaji wote hasa watoto na wanawake, vijana na wanaume wanaokumbwa na ukatili.
Katika ziara hiyo, CP Shilogile aliambatana na Mratibu wa Dawati la Jinsia na watoto Makao Makuu ya Polisi Dodoma, ACP Faidha Seleiman na Mratibu wa Polisi Dkt. Ezekiel Kyogo, ambao wote kwa pamoja walieleza kuridhishwa kwao na namna Mkoa wa Songwe unavyotekeleza kwa ufanisi majukumu ya Dawati hilo, huku wakisema ni mfano wa kuigwa na kuahidi kutoa ushirikiano wa karibu zaidi kwa maendeleo endelevu ya huduma hizo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la jinsia na watoto Mkoa wa Songwe, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Saada Salum aliahidi kuendelea kusimamia kikamilifu utendaji wa dawati hilo ili liendelee kutoa huduma kwa weledi, haki na uadilifu, huku akiongeza kuwa motisha hiyo kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi ni chachu ya kuongeza ari ya utendaji na kuhakikisha kuwa jamii inalindwa dhidi ya vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia.