Na Janeth Raphael MichuziTv- Dodoma.
Aliyekuwa Mbunge wa Tarime Mjini na Mtia Nia wa nafasi hiyo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka huu 2025 Michael Kembaki, amevunja ukimya baada ya jina lake kutoonekana katika orodha ya wagombea walioteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Kembaki, ambaye katika mchakato wa kura za maoni alipata kura 1,572 na kuibuka mshindi katika jimbo hilo, amesema kuwa licha ya mafanikio hayo, ameheshimu na kukubali maamuzi ya vikao vya chama ambavyo vilipitisha jina la mgombea mwingine(Ester Matiko).
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Agosti 25,2025 amesema,”Nawashukuru sana wananchi wa Tarime kwa kuniamini na kunipa kura zenu,lakini kama mnavyojua, utaratibu wa chama chetu hauishii kwenye kura za maoni pekee, mgombea hupatikana kupitia mchakato wa vikao mbalimbali vya chama,” amesema Kembaki.
Mwanachama huyo wa CCM amelezea msimamo wake, kuwa anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kulitumikia Taifa kwa miaka mitano iliyopita.
“Uongozi ni kupokezana, Mwaka 2020 nilikuwa wa pili kwenye kura za maoni lakini nikaaminiwa kupeperusha bendera ya chama,na sasa, niliyepita kura za maoni sikuteuliwa lakini nimepokea maamuzi ya chama kwa mikono miwili,” amesema kwa utulivu.
Kembaki amewaomba wafuasi na mashabiki wake kuungana na kumuunga mkono mgombea aliyeteuliwa na chama, akisisitiza kuwa sasa si wakati wa makundi wala malumbano bali ni wakati wa kujipanga kwa ajili ya ushindi wa CCM.
“Nawaomba wanachama wenzangu, mashabiki wangu na wananchi wa Tarime tuvunje makundi yote,Mgombea ameshapatikana, kilichobaki ni kumnadi kwa nguvu zote ili tushinde kwa kishindo,” amesema.
Amesema kuwa ahadi nyingi za maendeleo zilizotolewa na serikali ya awamu ya sita tayari zimetekelezwa kwa asilimia 85, na fedha nyingi zimeletwa wilayani humo kwa idhini ya Rais Samia. Hivyo ni wajibu wa kila mwanachama kuhakikisha serikali inaendelea kuaminiwa.
“Chama Hiki Hakina Upendeleo – Ushindani Wangu Ulinifanya Niwe Mbunge Mwaka 2020”amesema
Akiweka wazi kuwa hana kinyongo na mchakato wa chama, Kembaki ametoa mfano wa mwaka 2020 ambapo licha ya kuwa wa pili kwenye kura za maoni, CCM ilimteua kuwa mgombea na hatimaye akashinda ubunge.
“Nilipata kura 64, mwenzangu alipata zaidi ya 200, lakini bado chama kilinichagua,hii imenijengea imani kuwa CCM haina upendeleo bali inaongozwa na misingi imara ya kuchagua watu wasio na mawaa,” amesema.
Kembaki amesisitiza kuwa ataendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli zote za maendeleo, akiahidi kuwa bega kwa bega na mgombea aliyepitishwa na chama.
“Nitashiriki shughuli zote za maendeleo. Sasa ni muda wa umoja na maelewano. Chama kina utaratibu mzuri wa kupata wagombea tuendelee kuamini kuwa huu ni mchakato unaolinda heshima ya CCM,” amesisitiza.