Na Pamela Mollel, Arusha.
Zoezi la uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi ya ubunge nchini linaendelea kushuhudia sura mpya na za kuvutia, ambapo leo Jumatatu, Agosti 25, 2025, mwandishi wa habari mkongwe, Said Salim Njuki, amejitokeza rasmi kuchukua fomu ya kuwania ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.
Njuki alifika mapema katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Arusha Mjini, ambapo alipokelewa na maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) waliokuwa wakihudumia wagombea wanaojitokeza.
Zoezi la uchukuaji wa fomu lilianza rasmi Agosti 14 na linatarajiwa kukamilika Agosti 27, 2025, huku Watanzania wakielekeza macho yao kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.