Songea-Ruvuma.
Aliekuwa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro, leo Agosti 26, 2025 rasmi amechukua fomu ya kuwania ubunge wa jimbo hilo kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi, akiahidi kuendeleza utumishi uliotukuka kwa wananchi kwa misingi ya uadilifu na mshikamano.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu Dkt. Ndumbaro amesema kuwa ni kawaida kipindi cha uchaguzi ndani ya chama kuwa na makundi lakini baada ya uteuzi kufanyika na Halmashauri Kuu ya CCM kumteua mgombea mmoja, ni wajibu wa wanachama wote kuungana na kumuunga mkono alieteuliwa kwa ajili ya ushindi wa chama.
“Baada ya mchakato wa ndani kumalizika, kila mwana-CCM anapaswa kumuunga mkono mgombea alieteuliwa na chama, kinyume chake ni usaliti kwa chama na kwa misingi ya umoja wetu,” alisema Dkt. Ndumbaro.
Ameeleza kuwa nia yake haikuwa kugombana na mtu yeyote katika mchakato wa kuwania uteuzi, bali ni kutimiza haki yake ya kidemokrasia ndani ya chama, na sasa anaelekeza nguvu zake katika kuimarisha mshikamano na kuandaa kampeni ya ushindi.
Dkt. Ndumbaro amesema kampeni zitakazofanywa zitakuwa za karibu na wananchi kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo “kampeni ya nyumba kwa nyumba, chumba kwa chumba, kitanda kwa kitanda na shuka kwa shuka,” akisisitiza kuwa CCM itafanya kampeni ya kishindo na ya kisasa.
Mapema hii leo, wanachama wa CCM kutoka Jimbo la Songea Mjini walijitokeza kwa wingi kushiriki maandamano ya amani ya kumsindikiza Dkt. Ndumbaro kuchukua fomu ya ubunge, maandamano hayo yaliongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Mjini pamoja na Katibu wa chama hicho, yakionesha mshikamano na nguvu ya umoja ndani ya chama.
Uchukuaji wa fomu wa Dkt. Ndumbaro unaashiria mwanzo rasmi wa safari yake ya kuwania muhula mwingine wa kulitumikia Jimbo la Songea Mjini, huku akibeba matumaini ya kuendeleza maendeleo na mshikamano miongoni mwa wananchi.