Meneja Shughuli wa Kampuni ya Premium Active Tanzania Makaka Shaban wa pili kushoto akiwa na wafanyakazi wa Kampuni hiyo kwenye moja la ghala la kuhifadhi Tumbaku
…….
Na Mwandishi Maalum, Namtumbo
KAMPUNI ya Premium Active Tanzania inayojihusisha na kununua Tumbaku katika Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma,katika msimu wa kilimo 2024/2025 imetoa dola 60,000 sawa na fedha za Kitanzania Sh.milioni 155 kwa ajili ya mikopo isiyokuwa na riba kwa wakulima ili kujenga mabani 310 ya kukausha Tumbaku.
Meneja Shughuli wa Kampuni hiyo Mkoa wa Ruvuma Makaka Shaban alisema,lengo ni kuwasaidia wakulima wazalishe Tumbaku bora inayokubalika kwenye soko la ndani na nje ya nchi,wapate fedha nyingi na kuwapunguzia gharama kubwa kwenye uzalishaji.
“Tunaamini kupitia mikopo hii tuna uhakika tutaboresha zao la Tumbaku ili kukidhi mahitaji ya soko la dunia,mabani haya yanatumia kuni kidogo tunataka wakulima walime kwa tija na kuondokana na umaskini kupitia zao hili la Tumbaku”alisema Makaka.
Alisema,wameajiri maafisa ugani zaidi 12 ambao wamesambazwa kwenye vijiji mbalimbali kupitia vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) wanaofanya kazi ya kutoa elimu na ushauri kwenye zao la Tumbaku ili wakulima wazalishe Tumbaku yenye ubora mkubwa.
Alisema,wataongeza maafisa ugani kulingana na idadi ya wakulima kwa kuwa afisa ugani mmoja anatakiwa kuhudumia wakulima 200 hadi 250 na kwa sasa kuna wakulima wakulima zaidi ya 2,000 wanaofanya biashara na Kampuni hiyo.
“kwa maafisa ugani tulionao wanatosheleza kabisa mahitaji ya kuhudumia wakulima wanaofanya biashara na kampuni yetu,lakini kukiwa na ongezeko la wakulima na sisi tutalazimika kuongeza maafisa ugani ili kuwasaidia wakulima wetu”alisema.
Naye Afisa kilimo wa Kampuni hiyo anayehudumia jumla ya vyama saba vya msingi vya ushirika Atway Msuya alisema,kazi kubwa wanayofanya ni kuwasimamia wakulima wa Tumbaku kuanzia hatua ya kupanda mbegu,kuotesha miche kwenye vitalu hadi hatua ya upandaji.
Alisema lengo ni kuwawezesha wakulima wa zao hilo kulima kwa tija kwa kuzalisha tumbaku bora inayokubalika kwenye sokoni la Dunia ili wapate fedha nyingi na kujikwamua na umaskini.
Msuya alisema,wamemaliza masoko ya Tumbaku lakini kwa sasa wameanza msimu mpya wa kilimo kwa kuandaa vitalu na kuwahimiza wakulima waanze kupanda mbegu mapema kwa ajili ya kupata mazao bora.
Mmoja wa wakulima wa Tumbaku anayehudumiwa na Chama cha msingi Rwinga Amcos Abubakar Jumanne Idd,ameipongeza Kampuni ya Premium Active Tanzania kutoa mikopo ya fedha na kusambaza maafisa ugani kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakulima wa Tumbaku.
Alisema,elimu na mikopo waliyoipata imewasaidia kuzalisha tumbaku iliyo bora na kupata elimu sahihi ya matumizi ya pembejeo zinazotumika kwenye zao hilo tufauti na miaka ya nyuma ambapo walikuwa wanalima kwa mazoea kutokana na kukosefu wa wataalam waliobobea kwenye zao hilo.
Idd alisema,awali kabla ya kuja kampuni hii ekari moja alikuwa anavuna kilo 650 hadi 700, lakini kutokana na elimu na mikopo iliyotolewa na kampuni hiyo sasa ekari moja anavuna kilo 1,000 hadi 1,500 na wakulima wamepata soko la uhakika na bei nzuri wanapofikisha tumbaku kwenye mnada.
“Mimi nimezaliwa na wazazi waliokuwa wanalima tumbaku,lakini walikataa tamaa kutokana na changamoto mbalimbali hususani kukosa soko la uhakika,hata hivyo kutokana na mafanikio tunayopata sisi vijana hata wazee waliosusa kulima wamerudi na uendelea na kilimo cha zao hilo kwa sababu ya kuwepo kwa soko la uhakika”alisema.