Na Diana Deus, Muleba.
MDAU wa maendeleo wilayani Muleba mkoani Kagera Mosses Kiduduye ametekeleza kampeni ya Mkuu wa mkoa huo Fatma Mwassa Ijuka omuka (kumbuka Nyumbani) kwa kurabati miundo mbinu ya shule na kukabidhi Vifaa mbalimbali kwa wananchi wa vijiji vya Nyakatenge Bilabo na Biija Nyakatanga ambavyo vina thamani ya Sh.milioni 270.
Kupitia kutekeleza kampeni amekabidhi madawati, Vifaa vya michezo na kujenga Visima viwili vya maji kwa wananchi wa vijiji hivyo na kueleza amefanya hivyo kama sehemu ya kurudisha fadhila nyumbani.
Wananchi wa wilaya ya Muleba wameshuhudia jitihada za maendeleo Kiduduye ambaye ametekeleza kampeni hiyo kwa vitendo kwa kukarabati shule tano kongwe za msingi na kuweka miundombinu katika shule hizo pamoja na kutoa Vifaa vya michezo ,kukarabati Ofisi za walivu na ujenzi wa vyoo ili Kuendeleza Ushindani wa kielimu Katika wilaya ya Muleba
Akikabidhi miundombinu na Vifaa hivyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Muleba Dk.Abel Nyamahanga , Kiduduye amesema alivutiwa na kampeni ya Mkuu wa Mkoa ,hivyo aliamua kutafuta fedha ili kufanya jambo la kukumbukwa katika jamii yake.
“Mama yangu ni Mwalimu nilianza kutembelea shule niliyosomea niliona uchakavu wa miundo mbinu niliweka malengo na Kubaini shule Tano kongwe Muleba ,lakini kuna vijiji viwili tangu tuzaliwe kuna shida ya maji ,hivyo nilisema nitaunga serikali mkono.
“Najisikijia faraja kuona nimefanya ushawishi na kukusanya Sh.milioni 270 na kuyatekeleza haya yote kama sehemu ya jamii na kuacha alama na kicheko kwa jamii yangu,”amesema Kiduduye
Ameongeza Serikali imefanya mambo mengi lakini sasa ni wakati wa jamii kufanya mambo mazuri ya kukumbukwa na zaidi kushirikiana na serikali kuigusa jamii moja kwa moja katika mahitaji yao ambapo alidai kuwa atakuwa mstari wa mbele kushawishi wadau na vijana ili kurudi Nyumbani na kuweka alama zao
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muleba Dk.Nyamahanga amefurahishwa na mdau huyo ambapo amekiri kupokea miundombinu iliyoboreshwa katika shule tano za wilaya ya Muleba ,Madawati na Vifaa vya michezo pamoja na kupokea miundo mbinu ya maji kwenye Visima viwili Ambavyo vitahudumia wananchi wengi katika wilaya ya Muleba
Aidha amewataka wananchi kuendelea kushawishi watoto wao kujenga utamaduni wa kurejesha fadhila nyumbani , kujenga umoja na kudai kuwa ofisi yake iko wazi na yuko tayari kupokea watu wote kuanzia mfuko mmoja wa simenti,dawati moja ,lishe ya watoto na Kila kitu kwa ajili ya maendeleo.
“Vitabu vitakatifu vinasema mkono unaotoa ndio unaobarikiwa tuna watu wengi waliofanikiwa , tuwahimize warudi nyumbani, warejeshe furaha katika jamii zao zilizowalea ofisi iko wazi.Tuendeleze mshikamano na tufanye kitu kwa jamii na pia kwa wilaya yetu.”
Kwa upande wake Ofisa Elimu Shule za msingi wilayani Muleba Angasirini Kwekwa amezitaja shule zilizokarabatiwa na mdau huyu na kurudi kuwa za kisasa kuwa ni shule ya Msingi Tukutuku ,shule ya Msingi ,Shule ya msingi Rubungo, Shule ya Msingi Buyango na shule ya Msingi Muleba ambapo miundombinu ya shule na ofisi zimekarabatiwa kisasa
Amesema uwepo wa mazingira ya shule na ukarabati wa ofisi za walimu unaongeza kujiamini na ufaulu katika shule ambapo ametoa mwito kwa walimu, wanafunzi na jamii kulinda miundombinu ya shule na kuitunza ili kuendelea Kusaidia vizazi vijavyo.