NIRC Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Bw. Raymond Mndolwa, amewataka watumishi wapya wa NIRC kutumia maarifa na ujuzi walionao ili kufanikisha malengo ya Tume na kuzingatia uadilifu katika utendaji.
Amesema kila mtumishi ana nafasi ya kipekee katika utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo, hivyo ni muhimu kuelewa kanuni na taratibu za utumishi wa umma, kuwa na maadili na uadilifu kwa maslahi ya Taifa.
Akizungumza wakati wa kufungua Mafunzo Elekezi kwa watumishi wapya wa NIRC walioajiriwa na Serikali hivi karibuni, Mndolwa amesema mafanikio ya Tume yanategemea mshikamano, weledi na utendaji bora wa kila mmoja kwa kuzingatia maadili na uadilifu.
Amefafanua kuwa kila mtumishi anapaswa kutambua kuwa kazi yake ni sehemu ya mchango mkubwa unaolenga kuboresha kilimo nchini kupitia miradi ya umwagiliaji.
“Tunaposhirikiana na kutumia ujuzi wetu kwa ubora, tunachangia moja kwa moja maendeleo ya kilimo na kuleta tija kwa taifa. Kila mtumishi hapa ana nafasi ya kipekee na jukumu lake linategemea wengine wote,” amesema.
Ameongeza kuwa, “Siyo tu tunafanya kazi kwa ajira yetu, bali tunajenga historia ya maendeleo ya Taifa,” amesema Bw. Mndolwa.
Aidha, amesisitiza kuwa kila mtumishi anapaswa kuwa muadilifu na kuwa na uwajibikaji mkubwa katika kazi yake ili kufikia azma ya Serikali ya kuimarisha sekta ya kilimo nchini.
Amefafanua kuwa ni muhimu kutunza rasilimali za umma na kuhakikisha vitendea kazi vya miradi ya umwagiliaji vinatumika kwa ufanisi. Amesema kwa kufanya hivyo, miradi ya Tume itakuwa endelevu na kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu.
Pia, ameeleza kuwa siri ya mafanikio ni kupenda kazi yako, kujifunza kila siku na kuwa muadilifu katika kila hatua unayoichukua, jambo linalojenga msingi thabiti wa mafanikio katika utumishi wa umma.
Amesisitiza kuwa miradi ya umwagiliaji inayotekelezwa na Tume inapaswa kudumu kwa muda mrefu zaidi ya miaka 20, hivyo kila mtumishi ana wajibu wa kusimamia utekelezaji wake kwa umakini ili kuwa na ubora unaohitajika.
“Usifikirie tu kufanikisha mradi, fikiria kuwa huo mradi unapaswa kuleta tija kwa wakulima, kuongeza tija ya kilimo, kukuza kipato cha wananchi na kuhakikisha kuwa uwepo wake unaishi kwa vizazi vijavyo,” amesema.
Aidha, amesema kuwa usimamizi bora wa miradi ni kipimo cha weledi na uadilifu wa mtumishi, jambo linalohimiza mshikamano na ushirikiano wa pamoja ndani ya Tume.
Mafunzo hayo ya NIRC kwa waajiriwa wapya ni ya siku tatu kuanzia Agosti 27 hadi 29, 2025, yakiongozwa na wakufunzi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma.
Aidha, mafunzo hayo yamelenga kuwaandaa watumishi wapya kuingia katika utumishi wa umma wakiwa na uelewa wa pamoja kuhusu wajibu wao, taratibu za kisheria na maadili ya kazi, ili kuongeza tija na ufanisi wa taasisi.
Pia, watumishi hao wapya watapata fursa ya kutembelea miradi ya umwagiliaji iliyopo Morogoro ikiwemo wa Dakawa, pamoja na kuandaliwa warsha maalum ya ukaribisho kabla ya kwenda vituo vyao vya kazi.