
Mahakama ya Mwanzo jijini Lagos, Nigeria, imemhukumu mwanamke anayefahamika kwa jina la Jennifer kulipa faini ya ₦450,000 (sawa na zaidi ya Shilingi 730,000 za Kitanzania), baada ya kupatikana na hatia ya kupokea fedha kwa udanganyifu.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama, Jennifer alipokea ₦30,000 (takribani Shilingi 490,000 za Kitanzania) kutoka kwa kijana aitwaye Emmanuel, aliyedai kumpa fedha hizo kwa ajili ya nauli ya kumtembelea nyumbani kwake. Hata hivyo, baada ya kupokea fedha hizo, Jennifer hakufika kama walivyokubaliana na baadaye alikata kabisa mawasiliano.
Emmanuel aliwasilisha malalamiko mahakamani akidai kuwa kitendo hicho kilikuwa ni aina ya utapeli wa kifedha. Baada ya kusikiliza ushahidi, Mahakama ilibaini kwamba hatua ya Jennifer ilikuwa ni udanganyifu na unyonyaji wa kifedha, hivyo ikamuamuru kulipa fidia kubwa zaidi ya kiasi alichopokea awali.
Hakimu aliyesikiliza shauri hilo alieleza kuwa visa vya utapeli wa “nauli za usafiri” vimekuwa vikiongezeka na vinachukuliwa kama aina ya uhalifu wa kimtandao, akisisitiza kuwa hukumu hiyo imelenga kuwa fundisho na onyo kwa watu wengine wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Kwa mujibu wa hukumu, Jennifer anatakiwa kulipa faini ya ₦450,000, na endapo atashindwa kufanya hivyo, atakabiliwa na adhabu nyingine za kisheria ikiwemo kifungo.