Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Prof. Maulilio Kipanyula, akisoma hotuba wakati wa Mahafali ya 11 yaliyofanyika Agosti 28, 2025, ambapo jumla ya wahitimu 111 walitunukiwa shahada mbalimbali za Umahiri na Uzamivu.
……
TAASISI ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imejivunia kutimiza malengo matano ya msingi iliyojiwekea, likiwemo eneo la utafiti na ubunifu, pamoja na usimamizi madhubuti wa programu za uatamizi wa teknolojia.
Akizungumza Agosti 28, 2025 jijini Arusha wakati wa Mahafali ya 11 ya taasisi hiyo, Makamu Mkuu wa Taasisi, Prof. Maulilio Kipanyula, alisema taasisi hiyo imepanua wigo wake wa kitaaluma kwa kutoa Shahada ya Umahiri katika Ubunifu na Usimamizi wa Ujasiriamali kupitia Shule Kuu ya Mafunzo ya Biashara na Sayansi za Jamii (BuSH), ambapo wahitimu wa kwanza kutoka shule hiyo walitunukiwa shahada kwa mara ya kwanza.
Jumla ya wahitimu 111 walitunukiwa shahada katika mahafali hayo, ambapo 71 walitunukiwa Shahada ya Umahiri na 40 walitunukiwa Shahada ya Uzamivu.
Prof. Kipanyula alieleza kuwa dhana ya kubiasharisha bunifu na teknolojia inayoendelezwa na NM-AIST inalenga kusaidia Serikali katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kukuza viwanda na uchumi wa nchi kwa ujumla.
“Tunawataka wahitimu wetu kuwa na mtazamo wa soko katika kila bunifu wanayoanzisha. Hadi sasa, zaidi ya bunifu 35 zimepata hatimiliki. Hatua inayofuata ni kuhakikisha zinabiasharishwa kwa tija na kuwa chanzo cha mapato kwa taasisi na taifa,” alisema Prof. Kipanyula.
Aliongeza kuwa usimamizi wa uatamizi, uhaulishaji wa teknolojia na ubia kati ya watafiti na sekta binafsi ni nguzo muhimu ya kuimarisha uchumi kupitia maarifa yanayotolewa na taasisi hiyo. Hata hivyo, alisisitiza kuwa mafanikio hayo hayawezi kufikiwa bila kushirikisha jamii.
Katika mwaka wa kwanza wa masomo, Prof. Kipanyula alisema NM-AIST imefanikiwa kudahili wanafunzi 250 wa shahada za umahiri na uzamivu, ambapo wengi wao walinufaika na ufadhili wa Samia Scholarship. Kupitia ufadhili huo, wanafunzi 50 wamepata mafunzo katika maeneo ya akili bandia (Artificial Intelligence) na Sayansi ya Takwimu (Data Science).
Aidha, alieleza kuwa taasisi hiyo imenunua vifaa vya kisasa vya maabara na imepata ithibati ya kimataifa, hatua inayowezesha utafiti wa kiwango cha juu kinachokubalika kitaifa na kimataifa, hususan kwa kushirikiana na viwanda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Taasisi, Balozi Maimuna Tarish, aliwahimiza wahitimu kutumia ujuzi walioupata kutatua changamoto za jamii, kuanzisha ajira na kushiriki kikamilifu katika mageuzi ya kiuchumi.
“Maarifa, ujuzi na ubobezi mlioupata lazima uwe chachu ya mabadiliko chanya kwa taifa. Muwe na moyo wa kujituma, mzingatie uadilifu, na mwe mfano wa kuigwa katika jamii,” alisema Balozi Tarish.
Wakati huo huo, mmoja wa wahitimu hao, Isaac Mengele, alishukuru kukamilisha masomo yake katika taasisi hiyo huku akieleza kuwa tafiti yake ilihusu kuenea kwa vinasaba vya kinga kwa ng’ombe wa maziwa dhidi ya ugonjwa wa maziwa, kwenye mashamba madogo ya ufugaji.
“Nitahakikisha matokeo ya tafiti yangu yanawasaidia wafugaji wa ng’ombe wa maziwa kufuga kisasa zaidi, kupunguza magonjwa, na kuongeza tija,” alisema Mengele.
Mlau wa Mahafali ya 11 ya Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Prof. Gabriel Shirima, akiongoza maandamano ya wanataaluma kuelekea sherehe za Mahafali, Agosti 28, 2025, katika kampasi ya Tengeru, Arusha. Jumla ya wahitimu 111 walitunukiwa shahada mbalimbali za Umahiri na Uzamivu.
Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Prof. Maulilio Kipanyula, akisoma hotuba wakati wa Mahafali ya 11 yaliyofanyika Agosti 28, 2025, ambapo jumla ya wahitimu 111 walitunukiwa shahada mbalimbali za Umahiri na Uzamivu.
Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Mhe. Omari Issa (kulia), akimtunuku mmoja wa wahitimu (kushoto) wa Shahada ya Uzamivu wakati wa Mahafali ya 11 ya taasisi hiyo, Agosti 28, 2025. Jumla ya wahitimu 111 walitunukiwa shahada mbalimbali za Umahiri na Uzamivu.
Wahitimu wa Mahafali ya 11 ya Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) wakiwa tayari kwa ajili ya kutunukiwa shahada zao na Mkuu wa Taasisi, Mhe. Omari Issa (hayupo katika picha).