Na James K. Mwanamyoto – Morogoro
Wakuu wa Sehemu za Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Mikoa na Wakuu wa Divisheni za Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Halmashauri wametakiwa kutafuta fursa za uwekezaji katika maeneo yao ya utawala ambazo zinazoendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Serikali za Mitaa Sehemu ya Fedha Bw. Mudrika Mjungu kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, wakati akifunga Mafunzo ya Uwekezaji na Viwanda kwa viongozi hao wa Mikoa na Halmashauri yaliyofanyika katika Ukumbi wa Edema mjini Morogoro.
“Fikirieni maeneo sahihi ya uwekezaji kwenye mikoa na halmashauri zenu katika zama hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia ili uwekezaji huo uibue vyanzo vipya vya mapato,” Bw. Mjungu amesisitiza.
Bw. Mjungu ameongeza kuwa, ulimwengu wa teknolojia unakwenda kasi hivyo ni lazima viongozi hao waainishe fursa zilizopo ambazo zinazoendana na kasi hiyo ya maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Bw. Mjungu amehimiza kuwa, nafasi waliyopewa viongozi hao ya kuwa Wakuu wa Sehemu za Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Mikoa na Wakuu wa Divisheni za Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Halmashauri nayo pia ni fursa wanayopaswa kuitumia kubaini maeneo ya uwekezaji katika viwanda na biashara.
Naye, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Viwanda na Biashara Mkoa wa Dodoma, Bi. Mwajabu Nyamkomola amesema watatumia fursa za uwekezaji zilizopo katika Mikoa na Halmashauri kama ilivyoelekewa ili watanzania wanufaike na fursa za uwekezaji katika viwanda na biashara.
Mnufaika mwingine wa Mafunzo hayo Bi. Donatila Vedasto ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Viwanda na Biashara Mkoa wa Singida amesema kuwa, wamejengewa uwezo wa namna ya kuwavutia wawekezaji katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kupata uelewa wa kuwekeza kupitia ubia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Wilaya ya Lindi Bw. Rojas Mashauri amesema kwamba mafunzo waliyopatiwa yamekuwa na tija kwao kwani yamewajengea uwezo wa kutumia fursa za uwekezaji zilizopo katika maeneo yao, hivyo hawatatumika tena kama watoza kodi.
Jumla ya washiriki 210 kutoka katika Sehemu na Divisheni za Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Mikoa na Halmashauri waliudhuria mafunzo hayo ya siku mbili ya Uwekezaji na Viwanda, yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji pamoja na WIzara ya Viwanda na Biashara.