Mwakilishi wa Mradi wa ClimateFiGS upande wa Tanzania, Dkt. Lusekelo Kasongwa, ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, akichangia mada leo, Agosti 28, 2025, wakati wa kuhitimisha mkutano wa siku tatu wa kujadili mgawanyo wa fedha za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, uliofanyika katika Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam.
Mchunguzi Mkuu wa Mradi wa ClimateFiGS kutoka Chuo Kikuu cha Amsterdam, Dkt. Ruth Carlitz, akifafanua jambo wakati wa kuhitimisha mkutano wa siku tatu wa kujadili mgawanyo wa fedha za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, uliofanyika leo Agosti 28, 2026 Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam.
Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivukutoka Chuo Kikuu cha Amsterdam Wangoi Kagomba (aliyesimama) akiongoza majadiliano wakati wa kuhitimisha mkutano wa siku tatu wa kujadili mgawanyo wa fedha za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, uliofanyika leo Agosti 28, 2026 Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam.
Wadau wa Mazingira, Watafiti kutoka vyuo vikikuu mbalimbali ndani na nje ya Nchi wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuhitimisha mkutano wa siku tatu wa kujadili mgawanyo wa fedha za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, uliofanyika leo Agosti 28, 2026 Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam.
…………..
Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Amsterdam pamoja wadau wa mazingira, wakiwemo watafiti kupitia Mradi wa ClimateFiGS, wameazimia kuandaa muhtasari wa mapendekezo ya sera zitakazoiwezesha Serikali pamoja na sekta binafsi kutenga rasilimali fedha kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Mradi wa ClimateFiGS, unaofadhiliwa na Chuo Kikuu cha Amsterdam, unalenga kuongeza uelewa juu ya upangaji na mgawanyo wa fedha kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ili kuimarisha mikakati dhidi ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Akizungumza Agosti 28, 2025, wakati wa kufunga mkutano wa siku tatu uliofanyika Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, mwakilishi wa mradi
wa ClimateFiGS upande wa Tanzania Dkt. Lusekelo Kasongwa, ambaye ni Mhadhiri chuoni hapo, ameeleza kuwa mkutano huo umeibua mijadala muhimu itakayosaidia kuunda muhtasari wa sera bunifu kwa mustakabali wa Taifa katika kulinda mazingira.
Dkt. Kasongwa amesema kuwa moja ya maeneo ya mjadala katika mkutano huo ilikuwa ni umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika kupanga bajeti ya Taifa kwa ajili ya kuyakabili mabadiliko ya tabianchi, kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi na serikali.
“Tunapaswa kuoanisha malengo ya wananchi na yale ya Serikali ili kufanikisha mipango ya kibajeti yenye tija na inayotekelezeka. Pia, ni muhimu wizara zinazohusiana na mazingira kushirikiana kupanga na kutekeleza bajeti shirikishi inayolenga kukabiliana na athari hizo,” amesema Dkt. Kasongwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa ClimateFiGS kutoka Chuo Kikuu cha Amsterdam, Dkt. Ruth Carlitz, amesema kuwa mkutano huo ni hatua ya mwanzo kuelekea mgawanyo endelevu wa fedha kwa ajili ya miradi ya tabianchi, huku akisisitiza umuhimu wa tafiti na utekelezaji wa mapendekezo ya kitaalamu.
Naye Mshiriki wa Mkutano huo kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dkt. Josper Katomero, amesema kuwa mkutano umefungua fursa za kitafiti, ukizingatia kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, huku tafiti zikiwa chache eneo hilo.
“Ni wakati wa vyuo vikuu na asasi za kiraia kushirikiana kitaifa na kimataifa kufanya utafiti wenye matokeo chanya kwa wananchi,” amesema Dkt. Katomero.
Ameongeza kuwa mkutano huo umeibua hoja za msingi kuhusu umuhimu wa kuhusisha bajeti ya kitaifa na mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hasa kwa sekta zinazoathirika moja kwa moja kama kilimo, ufugaji na uvuvi.
Aidha, amesisitiza kuwa washiriki wa mkutano wamefungua njia ya ushirikiano wa utafiti kati ya taasisi za elimu ya juu kutoka Afrika Mashariki, hatua inayolenga kuongeza ufanisi katika kusimamia fedha na miradi ya kimazingira.
Mkutano huo umewakutanisha washiriki kutoka vyuo vikuu mbalimbali vikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu Mzumbe, pamoja na watafiti wa mazingira, taasisi za kiraia na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA).