Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) Beda Msimbe.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) umevitaka vyama vya siasa, wagombea na wananchi kwa ujumla kudumisha amani na kufuata sheria katika kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu unaoendelea nchini.
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa Agosti 28, 2025 na Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbie, jumuiya hiyo imesisitiza kuwa utunzaji wa amani ni jukumu la kila mmoja, huku ikihimiza vyama vya siasa kuendesha kampeni zao kwa njia ya kistaarabu bila kuhatarisha mshikamano wa kitaifa.
“Tunaomba vyama vyote vya siasa vitumie kipindi hiki kueleza ilani zao kwa wananchi kwa njia ya ustaarabu na bila kuhatarisha amani tuliyonayo. Ni wajibu wa kila chama na kila mgombea kuhakikisha kampeni zinabaki kuwa chachu ya maendeleo na siyo chanzo cha migawanyiko,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, TBN imewahimiza wanachama wake zaidi ya 200 kutumia majukwaa yao ya kidijitali kutoa habari sahihi na za uwajibikaji, ili kusaidia wananchi kuelewa vyema ilani za vyama na wagombea wao, na hivyo kufanya maamuzi sahihi wakati wa kupiga kura.
Mtandao huo umeihakikishia Serikali kuwa uko tayari kushirikiana nayo katika kulinda utulivu wa nchi na kupiga vita taarifa za upotoshaji zinazoweza kuhatarisha amani ya taifa. Pia umetoa tahadhari kwa wananchi na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuepuka kusambaza habari za uchochezi au zisizo na ukweli.
Kwa mujibu wa TBN, blogu na mitandao ya kijamii vina nafasi muhimu ya kudumisha amani na mshikamano, hivyo wadau wote wanapaswa kutumia majukwaa hayo kuimarisha demokrasia, kuhimiza mshikamano na kuilinda Tanzania dhidi ya siasa potofu.