




…………..
NA BALTAZAR MASHAKA, MISUNGWI
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zimeendelea kuwa chachu ya maendeleo nchini, baada ya kukagua, kuzindua na kuweka jiwe la msingi katika miradi mbalimbali ya kijamii wilayani Misungwi, mkoani Mwanza.
Miradi hiyo yenye thamani ya shilingi bilioni 2.57 inahusisha sekta za afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara, klabu ya wapinga rushwa, uchomeleaji na nishati safi ya kupikia.
Akizungumza wakati wa shughuli hizo, leo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, Ismail Ali Ussi, alisema miradi hiyo imetekelezwa kwa ubora wa hali ya juu na inaonesha dhamira ya kweli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha maisha ya wananchi wa Misungwi.
“Serikali inatekeleza miradi kulingana na mahitaji kwa gharama kubwa. Wananchi mnapaswa kuonesha mapenzi na imani kwa Rais Samia kwa kuunga mkono juhudi hizi na kulinda miundombinu hii ili idumu kwa zaidi ya miaka 20,” alisemai.
Ussi alisisitiza kuwa mafanikio makubwa yamepatikana chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, akitoa mfano wa miradi mingi ya barabara kwa kiwango cha lami inayotekelezwa mijini na vijijini kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), pamoja na miradi ya elimu, afya na maji.
Katika hatua ya kuimarisha elimu, Mwenge wa Uhuru ulizindua Shule ya Sekondari Mwasonge, ambayo ujenzi wake umegharimu zaidi ya shilingi milioni 714, zikiwemo nguvu za wananchi.
Shule hiyo imejengwa ili kupunguza adha ya wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali wa hadi kilomita 24 kufuata elimu katika vijiji vya jirani.
Aidha, Ussi alizindua madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Jitihada, yaliyojengwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani, huku akisema serikali ya awamu ya sita inalenga kuhakikisha darasa moja halizidi wanafunzi 40, ili kuongeza ubora wa elimu.
“Katika serikali ya awamu ya sita, hakuna sababu kwa mwananchi kuhoji upatikanaji wa maji, barabara au vyumba vya madarasa. Deni la imani hulipwa kwa imani, na deni la fedha hulipwa kwa fedha,” aliongeza.
Katika sekta ya afya, Mwenge wa Uhuru ulizindua jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika Zahanati ya Nyamikoma, ambalo limegharimu shilingi milioni 127.8, fedha hizo ni pamoja na shilingi milioni 40 za mapato ya ndani ya halmashauri, nguvu za wananchi zenye thamani ya milioni 17.8, na mchango kutoka serikali kuu.
Kiongozi huyo alieleza kuwa Mwenge wa Uhuru mwaka huu wilayani Misungwi umehusika katika uzinduzi wa miradi mitano, kukagua mradi mmoja, na kuweka jiwe la msingi katika mradi mmoja.
Ussi aliwataka wananchi kuonesha imani na mapenzi kwa Rais Dkt. Samia kwa vitendo ifikapo Oktoba 29, 2025, kwa kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya kuendeleza maendeleo.
“Oktoba 29 ni siku ya kipekee ya kuonesha mapenzi na imani kwa Dkt. Samia. Tuchukue nafasi hiyo kumuunga mkono ili aendelee na safari ya maendeleo zaidi ya tunayoyaona leo,” alisema.