

Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kigamboni, Bi. Tumaini Mahwaya akizungumza na wananchi wa Kata Kisarawe II leo 29 Agosti, 2025 wakati akitoa elimu ya masuala mbalimbali ikiwemo matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na ulinzi wa miundombinu ya umeme. (PICHA NA NOEL RUKANUGA)


Afisa Msaidizi wa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Kigamboni, Bi. Jamilah Masonga akitoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi wa Kata Kisarawe II, Manispaa ya Kigamboni.


Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Wilaya ya Mikwambe Mkoa wa Kigamboni Bw. Godwin Marandu akitoa elimu ya matumizi sahihi ya vifaa vya umeme pamoja na utaratibu wa kuomba kupata huduma ya umeme kwa wananchi wa Kata Kisarawe II, Manispaa ya Kigamboni.


Afisa Msaidizi wa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Kigamboni, Bw. Julius Vicent akitoa elimu ya ya umuhimu wa kulinda miundombinu ya umeme kwa wananchi wa Kata Kisarawe II, Manispaa ya Kigamboni.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Lingato, Kata ya Kisarawe II, Manispaa ya Kigamboni, Bw. Cosmas Sombi akiwakaribisha Maafisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Kigamboni, wakati walipofika katika mtaa huo kwa ajili ya kutoa elimu.

Wananchi wa Mtaa wa Lingato, Kata ya Kisarawe II, Manispaa ya Kigamboni wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Kigamboni.





Picha za matukio mbalimbali.
……….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kigamboni limewajengea uwezo wakazi wa Kata ya Kisarawe II kwa kuwaelimisha kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, umuhimu wa kulinda miundombinu ya umeme, na njia bora za kuwasiliana na Shirika kupitia namba 180 ili kuhakikisha wateja wake wanapata huduma bora ya umeme ya uhakika na endelevu.
Akizungumza leo, Agosti 29, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa utoaji wa elimu kwa wakazi wa Mtaa wa Lingato, Kata ya Kisarawe II, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Kigamboni, Bi. Tumaini Mahwaya, amesisitiza umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia kwani ni salama kwa mazingira na ina gharama nafuu kwa watumiaji.
Bi. Mahwaya amesema kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia ni muhimu si tu kwa afya za wananchi, bali pia kwa kulinda mazingira.
“Tunawahimiza wananchi kuacha matumizi ya kuni na mkaa na badala yake watumie umeme kwa kupikia, ili kupunguza uharibifu wa misitu na pia kujikinga na magonjwa ya mfumo wa upumuaji yanayosababishwa na moshi wa kuni, kupikia umeme ni rahisi na nafuu zaidi kuliko nishati zingine, amesema Bi. Mahwaya.
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Wilaya ya Mikwambe Mkoa wa Kigamboni Bw. Godwin Marandu, amesema kuwa
umuhimu wa kuzingatia usalama wa umeme majumbani na kutoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanaepuka matumizi hatarishi,
“Ni muhimu kutumia vifaa vya umeme kwa usahihi, ni hatari kuunganisha umeme kiholela vinaweza kusababisha ajali kubwa,”
Afisa Msaidizi wa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Kigamboni, Bw. Julius Vicent, ameeleza hatua zinazopaswa kufuatwa na mteja mpya anayetaka kuunganishiwa umeme, akibainisha kuwa kuna mfumo rasmi na rahisi wa kuwasilisha maombi.
“Tumeeleza jinsi ya kujaza fomu za maombi, pamoja na muda wa kusubiri kufikishiwa huduma. Tunataka kila mwananchi ajue hatua hizi ili kuepusha matapeli na vishoka,” amesema Bw. Vicent.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Lingato, Kata ya Kisarawe II, Manispaa ya Kigamboni, Bw. Cosmas Sombi, ameishukuru TANESCO Mkoa wa Kigamboni kwa kutoa elimu hiyo kwa wananchi na kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya umeme wakati wote, huku akihaidi kuwa balozi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia miongoni mwa wananchi wa eneo hilo.
Nao wakazi wa Mtaa wa Lingato wameipongeza TANESCO kwa kufika katika mtaa huo kutoa elimu hiyo muhimu, huku wakieleza kuwa mafunzo hayo yameongeza uelewa kuhusu matumizi salama ya umeme .
Kupitia mkutano huo wa elimu kwa umma, wananchi walipata nafasi ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kutoka kwa maafisa wa TANESCO Mkoa wa Kigamboni kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo huduma ya umeme, utaratibu wa kuunganishiwa umeme mpya, malipo ya bili, pamoja na namna ya kutoa taarifa pindi kunapotokea hitilafu au uharibifu wa miundombinu ya umeme katika maeneo yao.
TANESCO Mkoa wa Kigamboni imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuwahudumia watanzania kwa weledi na uwazi, huku ikisisitiza ushirikiano kati ya shirika hilo na wananchi kama nguzo muhimu ya kufanikisha upatikanaji wa huduma bora, salama na endelevu ya nishati ya umeme nchini.