

Katika siku ya kwanza ya Ziara ya Makamu wa Rais Zimbabwe, viongozi hao wameongoza Ujumbe wa Tanzania na Jamhuri ya Zimbabwe katika mazungumzo rasmi ambayo yamelenga namna ya kukuza uhusiano na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.

Mazungumzo hayo yamegusia zaidi urafiki wa muda mrefu wa kihistoria baina ya Tanzania na Zimbabwe tangu enzi za harakati za ukombozi wa Taifa la Zimbabwe, ambapo Tanzania chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilitoa msaada wa hali na mali kwa wapigania uhuru wa Zimbabwe.
Tanzania na Zimbabwe zimekubaliana kuendeleza uhusiano uliopo pamoja na kutunza historia ya mataifa hayo. halikadhalika majadiliano hayo yamelenga namna ya kukuza ushirikiano wa kiuchumi kwa kuzingatia muktadha dunia ya sasa ambapo ushirikiano kati ya mataifa umejikita kwenye masuala ya kiuchumi. Maeneo ya kiushirikiano ya uchumi yaliyoangaziwa ni pamoja na madini, kilimo, utalii, elimu pamoja na afya.

Vilevile Tanzania na Zimbabwe zimekubaliana kuwahamasisha wananchi kutumia fursa ya Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) pamoja na Soko Huru la Biashara la SADC ili kukuza biashara kati ya mataifa hayo. Aidha, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewakaribisha wafanyabiashara wa Zimbabwe kununua bidhaa zinazozalishwa kwa wingi hapa nchini, ikiwemo mchele, mabati na saruji. Vilevile, kuwakaribisha wawekezaji kutoka Zimbabwe kuwekeza nchini Tanzania.
Pia Tanzania na Zimbabwe zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika masuala ya kimataifa yenye maslahi kwa mataifa yote mawili ikiwa ni pamoja na kuendelea kupinga vikwazo ilivyowekewa Jamhuri ya Zimbabwe.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mheshimiwa Mohadi, yuko nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 30 – 31 Agosti 2025.
Ziara ya Mheshimiwa Mohadi nchini inalenga kuendelea kuimarisha uhusiano wa muda mrefu na wa kidugu na ushirikiano kati ya Tanzania na Zimbabwe katika maeneo yenye maslahi ya pamoja.
Tanzania na Zimbabwe zilianzisha uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1980 baada ya uhuru wa Zimbabwe. Uhusiano huo ulizidi kuimarika baada ya na kuanzishwa kwa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPCC) mwaka 1982, ambayo imeendelea kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali kama vile ulinzi, biashara, kilimo, utalii, madini, afya, elimu, na utamaduni.
Tanzania na Zimbabwe zinashirikiana katika maeneo ya usafirishaji, kilimo, madini, utalii, ulinzi na usalama, elimu, afya, sayansi na teknolojia, TEHAMA, mazingira na mabadiliko ya tabianchi, uhamiaji, utamaduni, michezo na sanaa.
Katika eneo la biashara na uwekezaji takwimu zinaonesha kuimarika kwa uhusiano wa kiuchumi ambapo Tanzania imekuwa ikiuza bidhaa zaidi nchini Zimbabwe na biashara hizo zimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 21.1s wa mwaka 2017 hadi kufikia Shilingi Bilioni 115.9 kwa mwaka 2023.