Wa kwanza kushoto ni balozi wa uvuvi wakati akikabidhi nyavu za kisasa kwa wavuvi kata ya kipili
Baadhi ya viongozi walioshiriki katika zoezi hilo la ugawaji wa nyavu za kisasa
………….
Na Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa:Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendelea na zoezi la ugawaji wa nyavu za kisasa kwa wavuvi wadogo wadogo kama sehemu ya juhudi za kukuza uchumi wa bahari na kuendeleza maisha ya jamii za wavuvi.
Zoezi hilo limefanyika katika kijiji cha kipili kata ya kipili wilayani Nkasi Mkoani Rukwa.
Ambapo balozi wa kupinga uvuvi haramu Paschal Mwakatenya amekabidhi nyavu pisi sita ambazo zitatumika kwa muda wa siku sita hadi saba kwa majaribio.
Amesema kuwa katika majiribio hayo anaamini kuwa nyavu hizo zitaleta faida kubwa na zitazuia uvuaji haramu kwani zimetengenezwa kwa ubora na viwango vya kimataifa.
Akizungumza leo Agosti 30,2025 Mwakatenya amesema uvuvi haramu umekuwa tishio kubwa kwa mazingira na kupoteza Mazalia ya samaki na kuyumbisha uchumi kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
“Niwaombe wananchi ambao mnafanya shughuli hizi za uvuvi haramu kuacha mara moja kwani serikali inapata hasara kubwa kwa kupoteza mapato yatokanayo na mazao ya majini.” Amesema Mwakatenya.
Kwa upande wake afisa tarafa wa kata hiyo Angelina Wangao amesema kuwa ugawaji huo ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuinua sekta ya uvuvi, kuongeza uzalishaji wa samaki, na kupunguza uvuvi haramu.
“Nyavu hizi ni rafiki kwa mazingira na zitawasaidia wavuvi kuvua kwa tija bila kuathiri mazalia ya samaki.”amesisitiza
Aidha amesema kuwa serikali inatambua mchango wa wavuvi wadogo katika uchumi, ndiyo maana wanashirikiana nao kwa karibu zaidi ili kuwaongezea nguvu katika kazi yao.
Nao baadhi ya wavuvi waliopokea nyavu hizo akiwemo Twaha Msemvu ameeleza kuwa vifaa hivyo vitawasaidia kuongeza kipato na kuboresha maisha ya familia zao.
“Vifaa hivi ni muhimu katika ufanyaji wetu wa kazi za uvuvi na ninawashauri wavuvi wenzangu kuachana na uvuvi haramu kwani unahatarisha si tu maisha yetu bali hata maisha ya viumbe hivi ambavyo vinatuingizia kipato.” Amesema Msemvu.
Mzee Anuari Mkamba ameelezea matumizi ya nyavu haramu yanavyoharibu mazingira wakati wa uvuvi kuwa yanahatarisha Mazalia ya samaki kwa kuwa wanavua samaki ambao ni wadogo na wengine wakiwa wameharibika.
“Huu ni uharibifu mkubwa wa mazingira na hata wengine hutumia sumu kwa ajili ya kuvulia samaki jambo ambalo linahatarisha afya za watumiaji.”
Mpango wa ugawaji wa nyavu umefanyika kwa mikoa ya Rukwa ,Kigoma na Katavi huku ukilenga zaidi wanawake na vijana wanaojishughulisha na uvuvi.
Uvuvi haramu umegeuka kuwa janga kubwa la kiuchumi na kimazingira ambapo kila mwaka mataifa ya afrika mashariki yanapoteza zaidi ya dola za marekani millioni 415 kutokana na uhalifu wa majini ambapo Tanzania pekee inafikia hasara ya dola milion 142.8.