NIRC – Dodoma.
WATUMISHI wapya wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, (NIRC), wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwaamini na kuwapa nafasi nyingi vijana katika ajira za hivi karibuni.
Pia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), imewataka waajiriwa wapya kujiandaa kuwahudumia wananchi ili kutimiza lengo la Serikali la kuboresha kulimo nchini kwa kuongeza tija katika uzalishaji
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala NIRC Maria Itemba katika ziara ya watumishi hayo walipotembelea miradi ya Umwagiliaji ya DAKAWA Mkoani Morogoro, lengo likiwa ni kujifunza kazi zinazotekelezwa na taasisi hiyo.
“Tumewaleta mashambani ili mjue Tume inavyofanya kazi, huku hatuvai suti. Suti zenu inabidi mziache mjini, hapa ni kazi tu lengo ni kuwahudumia wakulima na kufikia azma ya Serikali ya kuongeza uzalishaji wa chakula nchini,” amesisitiza Maria.
Maria amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wake Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kilimo hivyo utendaji wa watumishi hao unapaswa kwenda sambamba na uwekezaji huo.
Naye Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Morogoro, Juma Matanga, amewataka waajiriwa hao wapya 52 kutoka kada mbalimbali waliotembelea miradi ya Tume, kutambua wajibu walio nao kwa jamii na namna Serikali ilivyo na matumaini na wataalamu hao katika kuleta tija sekta ya kilimo.
Amesema,Tume inatarajia kujenga uzio kuzunguka Shamba la Umwagiliaji Dakawa ili kulinda miundombinu ya Umwagiliaji katika mradi huo.
Aidha, Tume hiyo pia itajenga uzio maalumu katika skimu hiyo pamoja na ujenzi wa bwawa la kuhifadhi maji litakalowezesha wakulima kupata maji ya uhakika misimu yote Mwaka mzima
“Kwa muda mrefu Mkoa wa Morogoro umekuwa ukikabiliwa na migogoro kati ya wakulima na wafugaji, huku chanzo ikiwa ni kutafuta eneo la malisho
“Uzio huu utaongeza tija katika sekta ya kilimo, wakulima kupata maji ya uhakika kwa msimu wote, lakini pia kudhibiti uharibifu unaosababishwa na wafugaji wanaolisha mifugo kiholela,”amesema.
Mhandisi Matanga amesema changamoto kubwa wanayokutana nayo katika mradi huo kwa sasa ni uharibifu wa mazingira katika Mto Wami, kuhama kwa njia ya mto na kupungua kwa maji na kusababisha kukosekana kwa maji kwenye pampu na hivyo kusababisha hasara kwa wakulima.
Wakizungumza mara baada ya ziara hiyo watumishi hao wameishukuru Serikali kwa kuongeza ajira na kuwaamini vijana.
“Tunashukuru Rais Samia na Serikali kwa kutuamini vijana na kutupa nafasi katika ajira. Tunachoweza kuahidi ni bidii ya kazi na kuwahudumia wananchi kupitia kazi zetu,” amesisitiza Deogratias Simbila, afisa habari mpya.
Naye Kulwa Mbegu aliyeajiriwa katika nafasi ya Uhandisi wa Mazingira, amesema wana deni kwa Rais Dkt. Samia kwa imani yake, na kwamba amefurahishwa na namna Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inavyozingatia sheria za mazingira katika miradi yake.
“Nimejionea namna Tume inavyodhibiti mazingira, maporomoko na mafuriko, nimejifunza mengi kwa vitendo, nitaenda kutumia ujuzi nilio upata katika kazi zangu,”ameongeza.
Skimu ya umwagiliaji ya Dakawa iliyoanzishwa mwaka 1982 na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Chakula la Taifa (NAFCO), kwa kujenga banio na kuchimba mfereji mkuu we urefu wa mita 7,400 na mifereji nane ya upili.Skimu hiyo ina eneo la hekari 3,225.15 zinazo kwa umwagiliaji, huku eneo linalomwagiliwa kwa sasa na lenye miundombinu ni hekari 2,000.