
Kocha wa zamani wa Manchester United, Erik ten Hag, ameondolewa rasmi katika benchi la ufundi la klabu ya Ujerumani Bayer Leverkusen baada ya kusimama katika michezo miwili pekee ya Bundesliga.
Ten Hag (55), alijiunga na Leverkusen msimu huu wa kiangazi mara baada ya kufutwa kazi na United mwezi Oktoba mwaka jana, akitarajiwa kuanza upya maisha ya ukufunzi katika Ligi Kuu ya Ujerumani.
Hata hivyo, mambo hayakwenda kama ilivyotarajiwa. Uongozi wa Leverkusen umeeleza kuwa miezi michache iliyopita imeonyesha changamoto kubwa katika kujenga kikosi kipya kitakachoweza kufikia malengo ya klabu hiyo.
“Hakuna aliyetaka kuchukua hatua hii, lakini wiki chache zilizopita zimeonyesha ni vigumu kuunda timu mpya itakayofikia mafanikio tunayotarajia,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa Leverkusen, Simon Rolfes, kupitia tovuti ya klabu.
Hadi kufikia sasa, Leverkusen haijatangaza rasmi mrithi wa Ten Hag, lakini taarifa zinaeleza kuwa majina kadhaa makubwa yanapigiwa hesabu kuchukua mikoba hiyo ndani ya siku chache zijazo.