Na WAF, Lusaka- Zambia
Nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika wamekutana Lusaka Zambia kujadili masuala mbalimbali yenye lengo la kuboresha afya kwa nchi wanachama na agenda mojawapo ikiwa ni uimarishaji wa viwanda vinavyozalisha dawa ili nchi hizo zijitosheleze kwa dawa na kupunguza utegemezi.
Mkutano huo wa 75 uliofanyika kuanzia Agosti 24 hadi 27, 2025 ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt.Seif Shekalage ambaye alimwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama na kwa mara ya kwanza umefanyika chini ya Sekretarieti inayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa WHO Kanda ya Afrika Prof. Mohamed Janabi ambaye alichaguliwa hivi karibuni kuongoza Shirika hilo Kanda ya Afrika.
Katika Mkutano huo Dkt. Shekalaghe alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Zambia na kujadiliana kuhusu fursa mbalimbali za ushirikiano katika sekta ya afya.
Aidha Dkt. Shekalaghe alishiriki katika vikao vya pembeni na wadau muhimu wa maendeleo ikiwemo taasisi ya Gates Foundation Afrika ambapo mazungumzo yalijikita katika vipaumbele vya taasizi hiyo na dhamira yao ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha ubunifu, mifumo ya fedha pamoja na afua za afya nchini.
Pia Dkt. Shekalaghe alifanya kikao cha pembeni na Shirika lisilo la kiserikali la (UNITAIDS) ambalo limeeleza dhamira yake ya kushirikiana na Tanzania katika kusaidia viwanda vya ndani kwa utaalam pamoja na rasilimali fedha ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa za afya ndani ya nchi pamoja na kushiikiana na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).
Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo unadhihirisha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuimarisha sekta ya afya nchini kupitia ushirikiano wa kikanda, kimataifa pamoja na wadau wa maendeleo ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.