Spika wa Umoja wa Bunge la Visiwa vya Comoro Mhe. Moustadroine Abdou akiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alipotembelea Kliniki ya JKCI Oysterbay kwaajili ya kuona huduma zinazotolewa pamoja na kupata matibabu.
Spika wa Umoja wa Bunge la Visiwa vya Comoro Mhe. Moustadroine Abdou akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupata huduma za matibabu hivi karibuni katika Taasisi yo Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Kliniki ya Oysterbay hivi karibuni. (Picha na Hamis Mussa)
………
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
Spika wa Umoja wa Bunge la Visiwa vya Comoro Mhe. Moustadroine Abdou ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwekeza kikamilifu katika sekta ya afya na kuimarisha huduma za kibingwa hususan matibabu ya moyo.
Ametoa pongezi hizo hivi karibuni alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kupitia Kliniki yake ya Oysterbay ambako alishuhudia huduma zinazotolewa na pia kupata matibabu.
Mheshimiwa Moustadroine alisema amevutiwa na miundombinu ya kisasa iliyowekezwa katika taasisi hiyo, akibainisha kuwa inakidhi viwango vya kimataifa katika kutoa huduma za matibabu ya kibingwa.
“Nimefurahi leo nimetembelea JKCI Kliniki ya Oysterbay na kujionea namna ambavyo Serikali ya Tanzania imewekeza katika vifaa vya kisasa vya matibabu ya moyo na kuwasomesha wataalamu. Nimepata huduma bora na kugundua kuwa wataalamu wa afya hapa ni marafiki wazuri wa wagonjwa”, alisema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa JKCI Dkt. Angela Muhozya alisema taasisi hiyo imeendelea kutoa huduma za kibingwa kwa Watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali jambo linaloonesha dhamira ya Serikali ya Tanzania katika kuokoa maisha na kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi.
“Tunajivunia kuona viongozi wa kimataifa wakitembelea JKCI na kushuhudia huduma tunazotoa. Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wa Tanzania na jirani wanapata huduma bora za moyo kwa gharama nafuu na mazingira rafiki”, alisema Dkt. Anjela.
Aliongeza kuwa taasisi hiyo itaendelea kusomesha wataalamu na kuwekeza katika teknolojia za kisasa ili kuhakikisha huduma zinabaki kuwa za kiwango cha juu kimataifa.
Kwa mujibu wa Spika Moustadroine, Tanzania imeweka mfano bora wa uwekezaji katika afya ambao unaweza kuigwa na mataifa mengine barani Afrika.