Na Mwandishi wetu
Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Chuo Cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC), Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa chuo hicho, Profesa Ahmed Ame, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kutumia takwimu katika kutengeneza sera za maendeleo ya taifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Septemba 1, 2025, wakati wa ufunguzi wa semina kwa waandishi wa habari, Prof. Ame amesema Serikali imepanua wigo wa matumizi ya takwimu katika upangaji wa maendeleo na kusisitiza kuwa takwimu sahihi ndizo msingi wa maamuzi bora.
“Takwimu ni namba ambazo haziongopi. Zinawawezesha wananchi kuelewa kwa usahihi kile kinachofanyika,” amesema Prof. Ame.
Alibainisha kuwa waandishi wa habari ni kundi muhimu katika usambazaji wa takwimu, kwa kuwa wao ndio wanaowafikia walaji wakuu wa taarifa, hivyo takwimu zinazotumika katika vyombo vya habari lazima zitokane na vyanzo vinavyotambulika kisheria.
Aidha, Prof. Ame amesema chuo hicho kimekuwa kitovu cha mafunzo na utafiti, kikihudumia nchi mbalimbali za Afrika, huku wakati mwingine wakufunzi wake wakitumwa kufundisha nje ya Tanzania.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika, Dkt. Tumaini Katunzi, amesema chuo kimekuwa kikizalisha wataalamu wa kutosha kwa ngazi ya shahada na shahada za uzamili, jambo linaloonesha matunda ya safari ya miaka 60 ya uwepo wa taasisi hiyo.
“Miaka 60 ya chuo hiki ni safari ndefu ambayo sasa imezaa matunda makubwa katika matumizi na tafsiri ya takwimu kwa maendeleo ya nchi na bara kwa ujumla,” amesema Dkt. Katunzi.

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)