Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MATUMIZI ya nishati safi ya kupikia yamepata msukumo mpya jijini Mwanza baada ya baadhi ya wananchi kukabidhiwa zawadi walizojishindia kupitia kampeni ya “Gesi Yente” inayoendeshwa na kampuni ya Oryx Energies, kama motisha ya kuhamasisha ununuzi na matumizi ya gesi ya kupikia.
Hafla ya kukabidhi zawadi hizo imefanyika leo Septemba 2, 2025 Buhongwa, jijini Mwanza ambapo Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Nyamagana, Thomas Salala, alimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Amina Makilagi.
Kampeni hiyo inalenga kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha kila Mtanzania anapika katika mazingira salama na kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania wote kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Akizungumza katika hafla hiyo, DAS Salala amesema kampeni hiyo ni muhimu kwani inaunga mkono msukumo unaoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye tangu Novemba 2022 amekuwa kinara wa ajenda ya matumizi ya nishati safi barani Afrika.
“Nishati chafu kama kuni na mkaa siyo tu kwamba zinachangia uharibifu wa mazingira, bali pia huathiri afya za watumiaji wake, hasa wanawake na watoto. Hivyo tunahimiza matumizi ya gesi ambayo ni salama, nafuu kwa muda mrefu, na rafiki kwa mazingira,” amesema Salala.
Ameongeza kuwa elimu ya matumizi ya nishati safi inayotolewa na wadau imeanza kuleta matokeo chanya, ambapo wananchi wengi sasa wanaelewa manufaa ya gesi ya kupikia kwa afya na mazingira.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Mauzo na Masoko wa ORYX Tanzania, Shaban Fundi, amesema mwitikio wa wananchi katika matumizi ya gesi ya kupikia umekuwa mkubwa mijini na vijijini, lakini bado inahitajika hamasa zaidi ili matumizi hayo yawe endelevu.
“Tunaendelea kutoa motisha kwa wateja, ikiwemo kugawa mitungi bure na zawadi mbalimbali, ili kuhakikisha wananchi hawakai na mitungi majumbani bali wanaiendeleza kuitumia mara kwa mara,” amesema Fundi.
Amebainisha kuwa kila mteja anaponunua gesi ya Oryx hupata kuponi yenye zawadi mbalimbali ikiwamo pikipiki, baiskeli, majiko, sufuria, mabegi na chupa za maji.
Katika hafla hiyo, washindi watatu walikabidhiwa zawadi ambapo mmoja alipata pikipiki na wawili wakajinyakulia baiskeli.
Mshindi wa pikipiki, Maximilian Nyamoge, amesema uamuzi wake wa kutumia gesi ya kupikia ulitokana na urahisi wake ikilinganishwa na kuni na mkaa, pamoja na faida zake kiafya na kiuchumi.
Kampeni ya “Gesi Yente” ilianza Agosti 13, 2025 na inatarajiwa kuendelea katika maeneo mbalimbali nchini.
Awali, Februari 25, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan, akizindua usambazaji wa mitungi ya gesi na majiko banifu kwa bei ya ruzuku wilayani Muheza, mkoani Tanga, alisema Serikali itaendelea kutunga sera rafiki zitakazohamasisha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kwa bei nafuu kwa Watanzania wote.