Na Mwandishi wa OMH
Tanga. Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) hususan Bandari ya Tanga kwa ufanisi mzuri wa kukusanya mapato makubwa ikiwa ni matokeo ya kukamilika kwa mradi wa maboresho katika bandari hiyo.
Pongezi hizo zilitolewa na Msajili wa Hazina Jumatatu, Septemba 1, 2025, wakati wa ziara yake katika bandari hiyo kwa lengo la kukagua utendaji kazi wake.
Akiongea mara baada ya kupokea taarifa ya utendajikazi wa bandari hiyo, Bw. Mchechu alisema kuwa uwekezaji uliofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan uliogharimu kiasi cha Sh429.1 bilioni umefanya meli kubwa kuweza kutia nanga na shehena ya mzigo pamoja na mapato kuwa makubwa.
“Tutahakikisha kuwa sekta binafsi pamoja na sekta ya umma zinaungana katika kufanya uwekezaji mkubwa kwa ajili ya manufaa ya umma,” alisema.
Aidha, Bw. Mchechu aliwataka wafanyakazi wa Bandari ya Tanga na TPA kwa ujumla kuendelea kufanyakazi kwa bidii na kuwataka kuiona bandari hiyo kama eneo muhimu la Serikali katika uchumi wa nchi.
“Lakini pia niwasihi wafanyakazi wa bandari hii tuone ufahari kwani tupo sehemu ambayo ni jicho na mboni ya Serikali katika uchumi wa nchi hivyo lazima tuichukulie kama sehemu muhimu inayohitaji huduma zilizo bora na tija kwaajili ya maendeleo,“ alisema Mchechu.
Pia Msajili wa Hazina alisema kufanya kazi kwa bidii kutawezesha mapato kuongezeka na mapato yakiongezeka hata gawio la Taasisi za Umma litangezeka kwani malengo ni kufikia Sh2 trilioni.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania Bw. Plasduce Mbossa alisema kuwa uwekezaji uliofanyika katika Bandari ya Tanga umesaidia kuhudumia meli gatini kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake Meneja wa Bandari ya Tanga Bw. Masoud Athumani Mrisha alimhakikishia Msajili wa Hazina kuwa huduma katika Bandari ya Tanga itazidi kuimarika.