Na Meleka Kulwa-DODOMA
WAKATI Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan,akiendelea kuboresha upatikanaji wa umeme kila kona nchini, wadau nao wameendelea kuhamasika kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ili kuachana na matumizi ya nishati chafu.
Akizungumza katika kampeni hiyo leo Septemba 2,2025 jijini Dodoma Meneja kutoka Kampuni ya Positive Cooker Kanda ya Kati Bw.Eliud Swai,amesema lengo la kuhamasisha wananchi kutumia majiko janja yanayotumia umeme, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuunga mkono ajenda ya kitaifa ya matumizi ya nishati safi.
Bw. Swai, amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kuwashawishi Watanzania kuachana na mila potofu kuhusu matumizi ya umeme kupikia na badala yake kuanza kuamini kuwa ni nishati rafiki, nafuu na salama.
“Lengo letu ni kufanya kampeni ya kutunza mazingira. Tunahamasisha wananchi watumie umeme kwa sababu hivi sasa kila nyumba ya Mtanzania ina umeme, lakini wengi wanauhusisha zaidi na mwanga, friji au kuchaji simu. Tunataka watambue kuwa umeme ni nishati nafuu jikoni kwako,” amesema Bw. Swai
Aidha amebainisha kuwa majiko hayo janja yanatumia wastani wa nusu uniti hadi uniti moja kwa saa moja ya kupika, sawa na shilingi 180 hadi 350, hali inayothibitisha ufanisi wake wa gharama.
Hata hivyo amesema kuwa ujio wa teknolojia hiyo mpya utasaidia kuondoa utegemezi wa mkaa na kuni, hivyo kulinda afya za watumiaji na kuokoa misitu.
“Lengo letu ni kutoa elimu kwa kila Mtanzania ili aache kutumia mkaa na kuni. Hii ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono kampeni ya nishati safi ya kupikia na kumsaidia mama wa nyumbani apike bila kero wala gharama kubwa kwa kutumia majiko ya umeme,” ameongeza Bw. Swai.
Nao Baadhi ya wananchi waliohudhuria kampeni hiyo wamesema kuwa elimu waliyopewa imekuwa ya msaada mkubwa, ikiwakumbusha madhara ya matumizi ya nishati chafu na faida za kutumia umeme kupikia.
“Elimu tuliyopewa ni nzuri, inatukumbusha umuhimu wa kutumia majiko haya ya umeme. Zamani tulipokuwa tunatumia kuni na mkaa tulipata changamoto nyingi, ikiwemo kuchelewa kuiva kwa chakula, lakini sasa majiko janja yanaongeza kasi na urahisi wa kupika,” wamesema
Iwapo familia nyingi zitatumia majiko hayo, kasi ya ukataji miti itapungua na hivyo kuimarisha uhifadhi wa misitu, hatua itakayosaidia Tanzania kufikia malengo yake ya kupunguza hewa ya ukaa.