Na. OR-TAMISEMI,Pwani
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi. Pili Mnyema, amewataka Wakuu wa Idara na Vitengo wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha uadilifu na weledi katika usimamizi wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaokubalika.
Bi. Mnyema ametoa wito huo leo, Septemba 2, 2025, wakati akifungua awamu ya pili ya Mafunzo ya Uongozi kwa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere kilichopo Kibaha, mkoani Pwani. Mafunzo hayo yameratibiwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi (UONGOZI Institute).
Amesema baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni usimamizi dhaifu unaosababisha ucheleweshwaji wa miradi au ujenzi wa chini ya viwango, jambo linalodumaza maendeleo ya wananchi.
“Tunajua kwenye maeneo yetu tunatekeleza miradi ya aina mbalimbali, lakini usimamizi usioridhisha unasababisha mingine kutokamilika kwa wakati au kujengwa chini ya kiwango. Baada ya mafunzo haya, naamini kila mmoja ataimarisha usimamizi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora,” amesisitiza Bi. Mnyema.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa viongozi hao kufanya tathmini binafsi baada ya mafunzo, ili kubaini mapungufu yaliyokuwa yakijitokeza katika maeneo yao ya kazi na kuyarekebisha kwa vitendo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bi. Angelista Kihaga, amewahamiza washiriki kuyatumia mafunzo hayo kama kichocheo cha mabadiliko chanya, huku akisisitiza mshikamano na mshirikiano wa kikazi.
“Mafunzo haya yawasaidie kubadilika na kufanya kazi kama timu. Ni wajibu wenu kuwasimamia watendaji mliyopewa ili kuhakikisha dhamira ya Serikali ya kuboresha huduma kwa wananchi inatimia,” amesema Bi. Kihaga.
Mafunzo haya yanatarajiwa kuwajengea uwezo viongozi hao katika masuala ya usimamizi, uwajibikaji na uongozi, ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi na utoaji wa huduma za kijamii katika ngazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa.