Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Builders of Future Africa (BFA) ,Elisante Ephrahim akizungumza katika hafla hiyo jijini Arusha.
…………..
Happy Lazaro, Arusha
ZAIDI ya Wamama wadogo 180 kutoka jamii ya kifugaji katika kata ya Lemanyata mkoani Arusha wamenufaika na mradi wa ujasiriamali pamoja kujengewa uwezo wa kuweza kutoa maoni na kusikilizwa katika jamii.
Aidha wamama hao ni wale wenye umri chini ya miaka 18 na ambao wana mtoto asiyezidi miaka mitatu au awe mjamzito.
Akizungumza wakati wa matembezi kwa ajili ya kuazimisha mradi wa wamama wadogo wenye kauli mbiu ya :nimejifunza ,Nimeweza sasa Mniamini”,Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Builders of Future Africa (BFA) ,Elisante Ephrahim amesema kuwa mradi huo ni wa mwaka mmoja ambapo ulianza oktoba mwaka jana na ndo unaishia ukingoni.
“Kabla ya kutekeleza mradi huu tulifanya utafiti katika jamii hizi za kifugaji kwa mabinti hawa wadogo na tukagundua kuwa wengi wao wameolewa wadogo ama kuzalishwa kutokana na mila zao ila unakuta bado wanahitaji kujiendeleza kwa ajili ya baadaye hivyo kila mmoja alitaja anachotaka kufanya ndipo tukaanza kutekeleza mradi huo kulingana na mahitaji yao na kwa kweli wamenufaika kwa kiwango kikubwa sana kwani sasa wanaweza kujitegemea na kujitafutia riziki wao wenyewe kwa kile walichojifunza .”amesema Elisante .
Amesema kuwa, mwaka 2022 ilikuwa ni kipindi cha Covid ndipo walifanya huo utafiti huo katika kata tatu ambazo ni Mwandeti,Lengijave ,na Lemanyata na kuweza kukutana na wamama wadogo 382 katika kata hizo na kuweza kuzungumza na mabinti hao na kufahamu changamoto zao ndipo mradi ukaanzia katika kata ya Lemanyata lengo kuu likiwa ni kuzuia ongezeko la mabinti chini ya miaka 18 kutokupata ujauzito.
Elisante amesema kuwa ,baada ya mradi huo kufika ukingoni watawezeshwa mitaji pamoja na vifaa vya kujiendeleza ili waweze kujiendeleza katika ngazi mbalimbali kulingana na kile ambacho wamefundishwa ambapo baada ya mradi kukamilika.katika kata hiyo watahamia kata nyingine waliyofanya utafiti kwa ajili ya kusaidia hao wamama wadogo .
Kwa upande wake Meneja miradi wa shirika la BFA ,Daniel Msigwa amesema kuwa.
Shirika hilo linashirikiana na mashirika mengine mawili ambayo ni Little Prospect Foundation kwa kushirikiana na Her journey to school ambapo kwa pamoja ndio tunatekeleza mradi huo huku mfadhili mkuu akiwa ni shirika la CRVPF .”amesema Msingwa.
Msingwa amesema kuwa, mradi huo unafanya kazi kwenye kata ya Lemanyata yenye vijiji vitatu ambapo unalenga kutatua changamoto za mabinti hao wadogo ili waweze kujikwamua kiuchumi baada kupatiwa ujauzito wakiwa wadogo na kushindwa kuendelea na ndoto zao.
Amesema kuwa , mradi huo ambao unajibu matatizo yao unalenga kutoa mafunzo ya ujasiriamali ikiwemo ushonaji,kupika keki, kushona shanga, kutengeneza sabuni, elimu ya lishe pamoja na utunzaji wa fedha na vikundi.
Msingwa ameongeza kuwa , wamama hao wadogo wameweza pia kujengewa vituo vya malezi vya watoto wao wapatao 192 vinne kwa ajili ya watoto wao kwenye vijijini hivyo vitatu kwa ajili ya kuwawezesha kupata elimu ya awali pamoja na kupata lishe ambapo watoto wamekuwa wakienda kila siku.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Little Prospects Foundation, Fauster Muttani ambao wanashirikiana kutekeleza mradi huo amesema kuwa wengi wa wamama hao wadogo ndoto zao zilizimika mapema sana kutokana na kupata ujauzito wakiwa wadogo hivyo mashirika hayo kwa pamoja wakaja na mradi huo ambao unalenga kuleta mabadiliko kwa wamama hao katika jamii zao na hatimaye kuweza kubadilisha historia mpya.
Baadhi ya wanawake walionufaika na mradi huo Anna Thomas amesema kuwa, kupitia mradi huo wameweza kujiamini katika kutoa maamuzi kwenye familia zao ikiwa ni pamoja na kupata mafunzo hayo ya ujasiriamali ambayo yamewawezesha kujiajiri kwani hapo awali walikuwa wankaa nyumbani tu bila shughuli yoyote, hivyo wanashukuru sana mradi huo kwani umekuwa mkombozi katika jamii hiyo ya kifugaji.