NA WILLIUM PAUL, SAME.
ALIYEKUWA Mtia nia wa Ubunge katika Jimbo la Same mashariki kupitia Chama cha Mapinduzi, CPA Ruth Hassan amewataka Wanachama wa Chama hicho katika Jimbo hilo kuvunja makundi na kuwapambania wagombea wanaotokana na CCM washinde kwa kishindo.
CPA Ruth alitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni za Mbunge wa Jimbo hilo kupitia CCM, Anna Kilango Malecel iliyofanyika katika kata ya Maore ambapo alisema kuwa, kwa sasa ndani ya chama wameshapatikana Wagombea wa kupeperusha katika nafasi ya Rais, Wabunge na Madiwani hivyo ni jukumu la wanaccm kuwa wamoja kuzitafuta kura.
“Natambua katika mchakato wa kura za maoni kila mmoja alikuwa na kundi lake lakini sasa ni muda wa makundi yote kuvunjwa na kuwa na kundi moja la CCM tuhakikishe Wagombea wetu wanapata kura za kishindo kuanzia Rais, Mbunge na Madiwani katika Jimbo letu” Alisema CPA Ruth.
Kada huyo wa CCM, alitumia pia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi kwa jinsi walivompokea wakati amekuja kugombea na kudai kuwa CCM ni Chama chenye mchakato mzuri ya kuwachuja wagombea ili kumpata mmoja wa kupeperusha bendera na kupongeza kwa jinsi haki ilivyotendeka kuanzia vikao ngazi ya wilaya, mkoa na Taifa.
CPA Ruth ambaye pia ni Mhasibu katika chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine ameahidi agenda yake ya kuhakikisha wananchi wa Jimbo hilo wanalima kilimo cha mkakati atashirikiana na Mbunge Anna pindi atakapochaguliwa kuhakikisha agenda hiyo inatekelezeka kwa vitendo.
“Wananchi tunawajibu wa kutambua kuwa mapinduzi ya kilimo yanapatikana ndani ya CCM hivyo nitashirikiana na Anna Kilango kuhakikisha kilimo chetu kinakuwa na nitaendelea kutoa elimu ya kilimo bure ndani ya Jimbo letu” Alisema CPA Ruth.