Na Sophia Kingimali
Jamii imeshauriwa kujihusisha na ufugaji wa sungura kibiashara, kutokana na soko lake kuendelea kukua nchini pamoja na kuwa fursa ya kujikwamua kiuchumi.
Nyama ya sungura imetajwa kuwa na faida nyingi kwa watumiaji, ikiwemo kuimarisha ubongo wa watoto, misuli kwa watu wazima, na kusaidia changamoto za uzazi.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 3, 2025 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kampuni ya Saore inayojishughulisha na ufugaji wa sungura, Suleyman Rugarabamu, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu fursa walizokuja nazo katika kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.
Amesema kampuni hiyo inatoa mtaji kwa watakaochangamkia fursa hiyo, ambapo mtu mwenye eneo atajengewa banda la kufugia na kupewa sungura wa kuanzia. Pindi watakapokomaa na kufikia kuanzia kilo moja, kampuni itawanunua tena.
“Sisi kama Saore tumejipanga kuhakikisha tunawasaidia Watanzania wenzetu kujikwamua kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuwasomesha watoto wao kupitia biashara hii ya ufugaji wa sungura. Tunafanya kazi na makundi matatu; wasio na mtaji, walio na mtaji na wale wanaotaka kufuga lakini wamebanwa na majukumu. Sisi tutawafugia na wao watapata faida yao,” amesema Rugarabamu.
Ameongeza kuwa sungura wanaotolewa kwa wafugaji tayari wamekatiwa bima, hivyo mfugaji atakapopata hasara ya kufa kwa sungura, atapewa mwingine bure bila malipo yoyote.
Akizungumzia faida za ufugaji huo, amesema sungura mmoja ana uwezo wa kuzaa watoto kati ya sita hadi 16 kwa mara moja na anaweza kuzaa kila mwezi. Vilevile, mkojo na kinyesi cha sungura vina faida kubwa kwani navyo huuzwa.
Kwa upande wake, bondia wa ngumi nchini Karim Mandogo, ambaye pia ni sehemu ya hamasa kwa vijana, amewataka vijana kutumia vyema fursa hiyo kwa kujitokeza kwa wingi kuanza ufugaji wa sungura kibiashara.
Ameeleza kuwa baada ya kujua faida ya nyama ya sungura, ameahidi kuanza kuitumia angalau mara moja kwa wiki ili kuimarisha afya yake na kuwa imara zaidi anapopanda ulingoni.
“Vijana wenzangu jitokezeni kwa wingi Saore mje kuchukua fursa hii. Unapewa sungura kama mtaji, unajengewa banda, halafu wakikua wanakuja tena kuwanunua wao wenyewe. Aisee tusibaki nyuma. Kuanzia sasa hakuna bondia wa kunipiga, nitakula nyama ya sungura mara kwa mara ili misuli yangu izidi kuwa imara,” amesema Mandogo.
Kampuni ya Saore imekuwa ikijihusisha na ufugaji wa sungura tangu mwaka 2018 na tayari imewafikia watu zaidi ya 6,000. Awali walikuwa wanatoa fursa kifamilia na kirafiki pekee, lakini sasa wamefungua nafasi hiyo kwa jamii nzima ya Kitanzania.