Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Songwe
MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amewapongeza wakulima wote nchini hasa mikoa inayozalisha mazao kwani mwaka huu mazao ni mengi hasa mahindi na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya pili ndani ya Afrika.
Dk.Samia ameyasema hayo leo alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Songwe alipokuwa akiomba kura katika mkutano wa kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29,2025.
“Nataka niwapongeze wakulima wote wa watanzania lakini hasa mikoa inayozalisha chakula ,mwaka huu Tanzania imekuwa ya pili kwa uzalishaji mazao hasa mahindi ndani ya Afrika.
“Na tumezalisha tanı milioni 10 lakini kwa ujumla ukichanganya mpunga na mazao mengine tunaotoshelevu wa chakula kwa asilimia 128 na hii ni kazi kubwa na inatupa faraja kuwa yale …
“Tunayotoa katika ruzuku kama mbolea ya ruzuku, mbegu na mambo mengine wakulima wanatumia na wanazalisha kwa wingi.Nitumie fursa hii kuwapongeza wakulima wote watanzania”
Pia amesema kuwa Serikali itaendelea kutoa Mbolea ya ruzuku huku akiwahakikishia wananchi wa Songwe kuwa Mbolea ipo na itafika katika Mkoa huo.
“Nimewasiliiana na Waziri wa Kilimo ameaniambia mbolea imeingia ila bado kusambazwa,mbolea ya kupandia tumbaku imeingia bado kusambazwa na mbolea ya kupandia mazao ipo bado kusambazwa. Kwahiyo mbolea ya ruzuku ipo na itaendelea kusambazwa.”
Kuhusu mikutano ya kampeni katika Mkoa wa Songwe amesema mkoa huo umefunika kwa wingi wa wananchi waliojitokeza katika mkutano na imani yake mikoa mingine atakapopita yeye na mgombea mwenza wake wananchi watajitokeza kwa wingi.
“Hapa Songwe mengi yamesemwa , wabunge wamesema,Katibu Mkuu Mstaafu Daniel Chongolo amesema lakini yote yamenipa faraja Serikali kwamba imeitendea haki Songwe kwa ujumla wake
“Nimetoka Tunduma na pale nimesikia yaliyotendeka Tunduma na Momba lakini nimeona wabunge walivyokuwa wanajivuna kwa maendeleo yaliyofanyika.Tunduma nikaambiwa wao ndio hodari wa kujenga hospitali za ghorofa na shule za ghorofa.Lakini nimekuja Vwawa na majimbo mengine maendeleo ni tele kwa tele.”
Kuhusu ombi la barabara ya Kamsamba ,Rais Samia Suluhu Hassan amesema katika miaka mitano ijayo barabara hiyo inakwenda kujengwa huku akisisitiza mkakati wa Serikali ni kuhakikisha Wilaya zote zinaunganishwa na Makao makuu ya Mkoa na hiyo ni katika mikoa yote nchini.