Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Vwawa katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa Chama hicho mkoani Songwe tarehe 03 Septemba, 2025.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa huo, Juliana Shonza akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan uliofanyika Mbimba Vwawa mkoani Songwe.
………………
Na John Bukuku, Songwe
Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Songwe kuwa Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Mlowo–Kamsamba kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na kukuza shughuli za kiuchumi.
Dkt. Samia alitoa kauli hiyo leo Septemba 3, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Mbimba, Vwawa mkoani Songwe, baada ya kuombwa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa huo, Juliana Shonza.
“Songwe ni mkoa unaokua kwa kasi na ni lango kuu la biashara kwa mikoa ya nyanda za juu kusini. Tutakamilisha barabara ya Kamsamba pamoja na barabara nyingine zinazohusiana na shughuli za kilimo na biashara ili wananchi mpate urahisi wa kusafirisha mazao yenu,” alisema Dkt. Samia.
Mbunge Shonza, akizungumza kwenye mkutano huo, aliomba Serikali kuhakikisha barabara hiyo muhimu inakamilishwa kwa kiwango cha lami kwani imekuwa changamoto kubwa hasa wakati wa mvua na hivyo kukwamisha shughuli za biashara na usafirishaji wa mazao.
“Mheshimiwa Rais, wananchi wa Kamsamba wamekuwa na matumaini makubwa na uongozi wako. Tunakuomba barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami ili kuondoa adha kubwa inayowakabili wananchi na kusaidia kuinua uchumi wao,” alisema Shonza.
Aidha, Dkt. Samia aliahidi kuendelea kuboresha miundombinu mingine muhimu mkoani Songwe ikiwemo afya, maji na elimu, huku akiwataka wananchi kuendelea kuiamini CCM kwa kumpa kura za kishindo ili Serikali iendelee kufungua fursa zaidi za maendeleo kupitia uwekezaji katika sekta ya miundombinu.