
Klabu ya Simba imeendelea kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC na michuano ya kimataifa kwa kutambulisha rasmi usajili wa beki wa kati Wilson Nangu akitokea klabu ya JKT Tanzania.
Nangu, ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), amekuwa akitajwa muda mrefu kuhitajika na vilabu vikubwa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuongoza safu ya ulinzi na nidhamu ya kiuchezaji uwanjani. Hatimaye, Simba wamemvuta ndani ya Msimbazi kwa mkataba wa miaka miwili.
Kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii, Simba wamethibitisha usajili huo kwa kumkaribisha Nangu kama sehemu ya kikosi kipya kinachoundwa chini ya benchi la ufundi lililo na malengo ya kutwaa makombe makubwa ndani na nje ya nchi.
Kwa usajili huu, Nangu anatarajiwa kuongeza nguvu kubwa kwenye safu ya ulinzi ya Simba, ambayo msimu ujao itakabiliana na changamoto za Ligi ya Mabingwa Afrika na michuano ya ndani.