* Awataka Watanzania kuacha alama katika utumishi wao
* Asema Serikali iko pamoja na wafiwa katika kipindi hiki cha majonzi
*Askofu Malasusa ataka waumini kumshuhudia Kristo kwa vitendo
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ibada ya mazishi ya Askofu Mstaafu Dkt. Martin Fatael Shao aliyefariki Dunia Agosti 25, mwaka huu.
Akizungumza katika ibada ya mazishi Septemba 4, 2025 yaliyofanyika katika kijiji cha Lole, Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro Dkt. Biteko amesema Hayati Askofu Shao wakati wa uhai wake alifanya mambo mengi mazuri ya kukumbukwa hata baada ya kifo chake.
“ Mzee wetu, Hayati Askofu Shao ameanza kazi za kanisa akiwa kijana na amefanya kazi kubwa ambayo kila mmoja anaishuhudia leo, ameacha alama inayotokana na kazi aliyoifanya, amesema
“Mheshimiwa Rais amenituma niwaletee salamu zake za pole nyingi sana Wanafamilia, Viongozi wote wa Kanisa KKKT pamoja na ndugu jamaa na marafiki wote kwa na msiba” amesema
Amesema Serikali itakumbuka mchango wa Askofu Shao ambaye ametumikia Kanisa katika maisha yake tangu ujana wake na hata baada ya kustaafu ameendelea kuwa mshauri.
Amewahimiza waombolezaji kuendelea kuwa karibu na kushirikiana na wafiwa katika kipindi hiki cha majonzi huku akiwahakikishia kuwa Serikali iko pamoja nao hasa katika kipindi hiki cha majonzi.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT, Dkt. Alex Malasusa amewataka waumini kutumia msiba huu kumshukuru Mungu kwa ajili ya mtu kama hayati Askofu Shao ambaye alikuwa kielelezo cha maisha bora kwa wanadamu.
Ameongeza kuwa Hayati Askofu Shao akikuwa mnyenyekevu na msikivu hali ambayo amesema imeanza kutoweka miongoni mwa wanajamii
“wanyenyekevu kama Dkt. Shao wameanza kuwa hadimu katika jamii na Viongozi waliomtengeneza Hayati Dkt. Shao walifaulu sana… amefanya mambo mengi ndani na nje ya usharika” amesema Askofu Dkt. Malasusa.
Amefafanua kuwa Askofu Shao enzi za uhai wake akifanya kazi kubwa ya
uinjiliahaji ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa umahiri mkubwa.
“ Tusizoee misiba, kila msiba utupe nafasi ya kutafakari maisha yetu,” amesema Askofu Malasusa.
Ibada ya mazishi imehudhuriwa na maelfu ya waombolezaji na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, Mkuu wa Mkoa wa Kilimajaro, Nurdin Babu na Mgombea wa Urais kwa tiketi ya CHAUMMA, Salum Mwalimu.