Na Mwandishi Wetu, Arusha
Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) imesema ipo tayari kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika mapambano dhidi ya rushwa, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa JMAT, Dkt. Israel Ole Gabriel Maasa, mara baada ya kumalizika kwa warsha maalum kuhusu Rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, iliyofanyika jijini Arusha Septemba 3, 2025.
“Tunaipongeza TAKUKURU Mkoa wa Arusha kwa elimu hii waliyotupatia kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba. Kama kaulimbiu inavyosema: ‘Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu; Tutimize Wajibu Wetu’, basi ni jukumu letu pia sisi viongozi wa dini kuwafundisha waumini na jamii kwa ujumla umuhimu wa kutojihusisha na vitendo vya rushwa hususan kuelekea Uchaguzi Mkuu, ili tuendelee kuilinda amani ya Tanzania yetu,” alisema Dkt. Maasa.
Aidha, JMAT imesisitiza kuwa viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika kuhakikisha jamii inapata elimu ya maadili na kutambua madhara ya rushwa, ili taifa liendelee kudumisha amani na mshikamano.