




Wajasiriamali wa sekta ya utengenezaji wa keki wametakiwa kurasimisha biashara zao na kuzingatia ubora wa bidhaa wanazozalisha ili kuhakikisha usalama wa walaji na kujiinua kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Ofisa Maendeleo wa Jiji la Mwanza, Erica Stephen, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Jiji, Wakili Kiomoni Kibamba, wakati akifungua maonesho ya kwanza ya kihistoria ya Keki, Kanda ya Ziwa yaliyofanyika jijini Mwanza.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuwainua wananchi kiuchumi, hususan wajasiriamali. Ili mfanye kazi kwa uhuru na kupata fursa zaidi, ni muhimu kurasimisha biashara zenu,” alisema Erica.
Alifafanua kuwa Idara ya Maendeleo ya Jamii imepewa dhamana ya kutoa mikopo isiyo na riba kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, akisisitiza kuwa maonesho hayo ni jukwaa la kujifunza, kubadilishana uzoefu, kujitangaza na kupanua wigo wa masoko.
“Tujitahidi kuwa rasimisha biashara, tuzingatie ubora kwa afya za walaji na kuhakikisha huduma kwa wateja inazingatia muda. Kujitangaza ni muhimu, watu hawawezi kufahamu unachofanya kama hujajitangaza,” aliongeza Erica.
Alizishukuru taasisi za BRELA, SIDO, TBS na VETA kwa mchango wao mkubwa katika kuwawezesha wajasiriamali kwa kutoa mafunzo ya usimamizi wa biashara, udhibiti ubora na usajili wa majina ya biashara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya BJ Empire iliyoandaa maonesho hayo, Benard James, alisema tukio hilo ni la kihistoria kwani ni mara ya kwanza kwa sekta ya waokaji keki kupewa jukwaa kubwa Kanda ya Ziwa na nchini.
“Lengo letu ni kuipa sekta hii hadhi, kuiinua na kuikuza ili iweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya taifa. Kwa kushirikiana na serikali, tunaamini ukuaji wa sekta hii utapunguza changamoto ya ajira nchini,” alisema James.
Aliongeza kuwa maonesho hayo yameleta mwelekeo mpya katika sekta ya uokaji ambapo kabla, waokaji walipatiwa mafunzo ya uendeshaji na usimamizi bora wa biashara,utengenezaji wa keki kwa viwango vya kisasa, usajili wa biashara na udhibiti ubora wa bidhaa kupitia taasisi za VETA, SIDO, TBS na BRELA.
Baadhi ya wajasiriamali walioshiriki, akiwemo Aurelia Aristedes na Lina, walieleza furaha yao kushiriki maonesho hayo huku wakibainisha mafanikio na changamoto zinazowakabili.
“Maonesho haya yametufungua macho, tukipata mikopo isiyo na rba kutoka serikalini itatuepusha na mikopo ya kausha damu.Kupitia maonesha haya tutapata wateja wapya na kujifunza kwa wengine lakini ipo changamoto kubwa yawateja kuahirisha kuchukua oda,” alisema Aurelia.
Lina, naye aliongeza; “Biashara yangu inakua kwa kasi, lakini gharama za vifaa na mabadiliko ya bei ya mara kwa mara ni changamoto. Kukatika kwa umeme wakati wa kutengeneza keki kunasababisha hasara kubwa.”