Na Rashid Mtagaluka
Mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya siasa na kijamii nchini, Saleh Mohamed, amesema Tanzania ipo katika njia sahihi ya maendeleo na kwamba miaka mitano ijayo nchi itakuwa imepiga hatua kubwa zaidi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza Septemba 4, 2025 kupitia mahojiano na Radio Free Afrika jijini Dar es Salaam, Saleh alisema kuwa Rais Samia amedhihirisha uwezo wa kuongoza kwa matokeo, hivyo ni afadhali wananchi wakampatia nafasi ya kuendelea kuliko kujaribu viongozi wa majaribio.
“Tusichague viongozi wa majaribio, miaka 5 ya maisha yako iko mikononi mwako, usipozingatia ilani ya vyama na kiongozi utakuja kujilaumu bure”, alisema Saleh.
Alisisitiza kuwa ni busara kumpa madaraka mtu ambaye tayari ameonesha alichokifanya badala ya mtu anayetaka kujaribu, kwa sababu maisha ya miaka mitano yako mikononi mwa wananchi na maamuzi yasiyo sahihi huweza kuligharimu taifa lote.
Saleh alisema hatua ya kufanikisha upatikanaji wa umeme katika kila kijiji nchini imewezesha wananchi wengi kuanzisha miradi midogo ya kiuchumi ikiwemo saluni, mashine za kusaga nafaka na biashara ndogo ndogo, na hivyo kuongeza kipato cha kaya.
Akizungumzia sekta ya kilimo, Saleh alisema kilimo kimegeuka kuwa nguzo ya uchumi mpya, kikichangia wastani wa asilimia 27 ya pato la taifa kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya 2024.
Kuhusu mradi wa Building a Better Tomorrow (BBT), zaidi ya vijana 120,000 wamenufaika kwa kupata elimu na ujuzi wa kilimo cha kisasa na kwamba hatua hiyo imeondoa dhana ya kilimo cha makaratasi kisicho na tija na kukifanya kiwe chanzo cha ajira na kipato, huku hata matajiri wengi wakielekeza uwekezaji wao katika sekta hiyo.
Saleh alisisitiza kuwa kilimo kitaleta mageuzi makubwa ndani ya miaka mitano ijayo, hasa baada ya ongezeko la ruzuku ya mbolea lililowezesha kushuka kwa bei kutoka wastani wa shilingi 120,000 kwa gunia la kilo 50 mwaka 2021 hadi chini ya shilingi 70,000 mwaka 2024.
Aidha, mchambuzi huyo alibainisha kuwa changamoto ya masoko pia imepungua kwani mazao ya Tanzania sasa yanapata masoko katika nchi jirani kama Kenya, Uganda na Zambia, ambapo zaidi ya tani milioni 1.2 za mahindi na mazao mengine ziliuzwa nje ya nchi mwaka 2023 pekee.
Kuhusu elimu, Saleh alisema serikali imeongeza wigo kwa kuimarisha vyuo vya kati na VETA, ambavyo kwa sasa vinahudumia zaidi ya wanafunzi 250,000 nchini kote, sambamba na kuboresha mitaala inayowawezesha vijana kupata elimu yenye ujuzi unaohitajika katika maisha ya kila siku.
Alisema hatua hii ni uthibitisho wa faida ya kuwa na viongozi wa kaliba ya Rais Samia ambao wanajali maandalizi ya vijana kwa maisha ya sasa na ya baadaye.
Akihitimisha mahojiano hayo, Saleh aliwaonya Watanzania kutochagua viongozi wa majaribio katika uchaguzi mkuu ujao, akisema kufanya hivyo ni kujiwekea hatari binafsi na kuligharimu taifa kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa kama Watanzania wataendelea kumpa imani Rais Samia, hakuna shaka kwamba miaka mitano ijayo Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi za mfano barani Afrika kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wao baadhi ya wanachi waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi, wamepongeza utendaji kazi wa serikali ya awamu ya sita na kwamba, mchambuzi alikuwa sahihi kwa alichosema.
Kwa sasa jumla ya vyama 17 vimesimamisha wagombea wa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29,2025