Na Mwandishi Wetu
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umeahidi kuiwezesha Shule ya
Sekondari Kambangwa iliyopo Kinondoni Jijini Dar es Salaam kwa kuipatia vifaa muhimu vya kujifunzia zikiwemo kompyuta, kichapishi (printer) pamoja na kujenga uzio wa shule hiyo.
Ahadi hiyo imetolewa na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda wakati akihutubia katika Mahafali ya 26 ya Kidato cha Nne ya shule hiyo ambapo Bi. Mwenda alikuwa Mgeni Rasmi.
Mahafali hayo yaliyofanyika katika viunga vya shule hiyo yalianza kwa shamra shamra za kuwapongeza wahitimu zilizojumuisha burudani na maonesho mbalimbali ya kitaaluma na kisha kufuatiwa na risala ya wahitimu pamoja na taarifa ya shule iliyowasilishwa na Mkuu wa Shule, Mwl. Angelina Mwakalukila.
“Tunaishukuru serikali yetu kwa kugharamiwa masomo ya vijana wetu kupitia sera ya elimu bila malipo ikiwemo kutupatia vitabu vingi vya masomo ya sayansi vinavyoendana na sera ya ufundishaji wa mtaala mpya. Kwasasa hatuna upungufu wa vitabu,” alieleza
Mkuu wa Shule katika taarifa yake na kuongeza: “Ndugu Mgeni Rasmi palipo na mafanikio hapakosi changamoto kadhalika shule yetu inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa maktaba, kompyuta, kuchakaa kwa baadhi ya miundombinu ya madarasa pamoja na shule kushindwa kukamilisha ujenzi wa uzio wa shule.”
Akiwasilisha hotuba yake katika mahafali hayo, Mgeni Rasmi, Bi. Khadija Mwenda ambaye ni Mtendaji Mkuu wa OSHA, amewapongeza wahitimu kwa kufikia hatua hiyo muhimu.
Aidha, amewapongeza walimu, wazazi na walezi kwa kushirikiana kuwalea vizuri wanafunzi hao huku akiwasisitiza kujiandaa kikamilifu kwa mitihani yao mwisho itakayofanyika kuanzia mwezi ujao.
“Ninaungana na wazazi na walimu kuwatakia kila la heri katika mitihani yenu na inshallah Mwenyezi Mungu atawaongoza kufanya vizuri ili muweze kutimiza ndoto zenu.
Vile vile, natambua kwamba baadhi yenu mmefikia umri wa kupiga kura hivyo nitumie fursa hii kuwakumbusha na kuwahimiza kushiriki zoezi la kupiga kura ifikapo Oktoba 29 ili nchi yetu iweze kupata viongozi bora,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA.
Aidha, ameahidi kushirikiana na uongozi wa shule kutatua changamoto mbali mbali zilizowasilishwa na Mkuu wa Shule kupitia program ya kusaidia jamii (CSR programme) ya Taasisi yake.
“Serikali imetuagiza kutenga fedha kwa ajili ya kuchangia utatuzi wa changamoto mbalimbali katika jamii ambapo Taasisi ya OSHA kupitia sera yake ya kusaidia jamii, tutaisaidia shule hii kukamilisha ujenzi wa uzio pamoja na kuwanunulia kompyuta 10 na vichapishi (printers),” ameongeza Bi. Mwenda.
Wakitoa shukrani zao, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule, Bw. Mohamed Mawinda pamoja na Kiranja Mkuu wa Shule hiyo, Bw. Brian Shirima, wamemshukuru Mtendaji Mkuu na Taasisi ya OSHA kwa kuona umuhimu wa kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili shule hiyo ambazo zimekuwa zikiathiri ufanisi wa masomo na malezi bora ya maelefu ya wanafunzi wa shule hiyo.
Shule hiyo iliyoanzishwa mwezi Julai mwaka 1997 na kuzinduliwa rasmi na Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjam William Mkapa na inahudumia zaidi ya wanafunzi 1,300 kwasasa.


